Kesi ya uchaguzi inamkabali mbunge wa jimbo la Kigoma Mjini Calyton Chipando, maarufu kama (Baba Levo) inaendelea kusikilizwa leo Julai 8, 2026 katika mahakama kuu ya Tanzania, masijala ndogo ya Kigoma ambapo mashahidi wanaendelea kutoa ushahidi wao mbele ya jaji Victoria Nongwa.
Ikumbukwe kuwa waleta maombi katika kesi hiyo ni wananchi wapiga kura wanne wa jimbo la Kigoma Mjini ambao ni Johary Kabourou, Pendo Kombolela, Luma Akilimali na Loam Mwita.
Wananchi hao walifungua kesi dhidi ya Babalevo na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (CAG) kupinga ushindi wa mbunge huyo baada ya kutangazwa kuwa mshindi katika uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 2025 wakidai kuwa ulikuwa na kasoro.
Katika kesi hiyo namba 28949/2025, waleta maombi hao wanne wanapinga ushindi wa Baba Levo katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025, wakidai kuwa ulikiukwa kwa taratibu, sheria na kanuni za uchaguzi, pamoja na madai ya rushwa na udini.
Miongoni mwa mashahidi waliosikilizwa siku ya leo ni Pendo Kombolela mkazi wa Mwanga Kaskazini alieeleza mahakama jinsi ambavyo alishuhudia mawakala wa chama cha ACT Wazalendo walivyotolewa nje ya vituo vya kupiga kura katika vituo vinne tofauti.
Amedai kuwa wakati tukio hilo lilitokea wakati yeye akiwa katika foleni ya wapiga kura katika kituo namba tano na kwamba alipoingia ndani ya kituo cha kupiga kura aliona karatasi zikiwa zimechanwa na kugongwa muhuri jambo lililomtia mashaka.
Naye, shahid Luma Akilimali mkazi wa Kasingirima ameeleza kuwa alimuona mtu aliyemfahamu kwa jina moja la Mwantum kupitia mtandao wa Millard Ayo akiomba kura za Baba Levo majukwaani baada ya mgombea huo kumuahidi kumpatia kiasi cha Sh. milioni moja ya mtaji kwa masharti kuwa anapaswa kumuombea kura.
Kupitia maombi yao, wanaiomba Mahakama iamuru kufanyika kwa upekuzi na kuhesabiwa upya kwa kura zilizopigwa katika jimbo hilo na hatimaye kutengua matokeo ya uchaguzi yaliyompa ushindi Baba Levo.
Usikilizwaji wa ushahidi ulianza Jumatatu ya wiki hii kabla ya kusitishwa kwa mapumziko ya maadhimisho ya Sabasaba jana Jumanne.
Ushahidi wa kesi hii ulianza kusikilizwa Julai 06, 2026. Ina jumla ya mashahidi 16, mashahidi saba mpaka sasa wameshasikilizwa.
Kesi ina jumla ya mawakili sita wa serikali, wawili upande wa mshtakiwa ( Baba Levo na mmoja upande wa walalamikaji ( Wananchi)
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED