Kamati Bunge yatoa kongole TANESCO kwa Mradi wa Umeme Kishapu

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 07:33 PM Mar 13 2026
Kamati Bunge yatoa kongole TANESCO kwa Mradi wa Umeme Kishapu

Kamati ya Kudumu ya Bunge la Tanzania ya Nishati na Madini imelipongeza Shirika la Umeme Tanzania kwa usimamizi na utekelezaji mzuri wa Mradi wa Uzalishaji Umeme kwa Nguvu ya Jua wa Kishapu wenye uwezo wa Megawati 50.

Pongezi hizo zimetolewa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Subira Mgallu, baada ya ziara ya mradi huo leo Machi 13, 2026, ambapo Kamati ilijionea maendeleo ya utekelezaji wake na ufanisi wa matumizi ya fedha zilizotolewa na Serikali.

Mgallu amesema mradi huo ni hatua muhimu katika mageuzi ya sekta ya nishati nchini kutokana na matumizi ya teknolojia ya nishati jadidifu. “Tanzania kwa mara ya kwanza inapata Megawati 50 za umeme kutoka kwenye nishati ya jua,” ameongeza.

Amesema Kamati imeridhishwa na namna fedha za Serikali, takribani shilingi bilioni 118, zimetumika ipasavyo kufanikisha mradi huo. Aidha, mradi tayari umeanza kuchangia Megawati 50 katika Mfumo wa Gridi ya Taifa Tanzania, hatua inayoongeza uhakika wa upatikanaji wa umeme.

Kwa upande wake, Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi, amesema mradi wa Kishapu unatekelezwa kwa awamu mbili; awamu ya kwanza ya Megawati 50 tayari imekamilika na kuanza kuingiza umeme katika Gridi ya Taifa, huku awamu ya pili ikihusisha uzalishaji wa Megawati 100 zaidi, kufanya jumla ya Megawati 150 kutoka mradi huo.

Kamati pia imetoa rai kwa Wizara ya Nishati na TANESCO kuhakikisha mikakati ya kuanza utekelezaji wa awamu ya pili inafanikishwa ili kuongeza zaidi uwezo wa uzalishaji wa umeme nchini.