JKT yapongezwa kwa kutoa ajira kwa vijana

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 03:58 PM Jul 07 2026
JKT yapongezwa kwa kutoa ajira kwa vijana
Picha: Mpigapicha Wetu
JKT yapongezwa kwa kutoa ajira kwa vijana

WAZIRI wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Dk. Rhimo Nyansaho, amesema Shirika la Uzalishaji Mali la JKT (SUMAJKT), linaendelea kutoa mchango kwa nchi, hasa kupunguza tatizo la ajira kwa vijana kupitia kampuni zake tanzu.

Amesema hayo alipotembelea banda la JKT katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa (DITF) maarufu Sabasaba, yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, Barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam.

Dk. Nyansaho amesema kampuni tanzu za SUMAJKT zimeendelea kufungua fursa za ajira kwa maelfu ya vijana, akitolea mfano Kampuni ya Usafi na Unyunyizi Dawa ya SUMA JKT (SUMAJKT Cleaning and Fumigation Company Limited), ambayo imetoa ajira kwa zaidi ya vijana 4,000 wa Kitanzania.

Pia amesema Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na JKT, vinaendelea kutekeleza kwa ufanisi majukumu yake ya ulinzi na uzalishaji mali, hatua inayochangia kuimarisha usalama wa taifa na kuwawezesha wananchi kutekeleza shughuli zao za maendeleo kwa amani.

Amesema wananchi wanapaswa kutembelea banda la JKT katika maonesho hayo, ili kujionea na kufahamu shughuli mbalimbali zinazotekelezwa na jeshi hilo kupitia vikosi, makambi, shule, chuo pamoja na huduma na biashara zinazotolewa na kampuni tanzu za SUMA JKT.