Daktari Bingwa wa Uzazi na Magonjwa ya Wanawake katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini (KCMC), Dk. Tomy Kakumbi, amesema uwezo wa mwanaume kufanya tendo la ndoa mara nyingi hauwezi kutumika kama kigezo cha kuthibitisha uwezo wake wa kumpa mwanamke ujauzito, akisisitiza kuwa uchunguzi wa kitabibu ndio njia pekee ya kubaini uwezo halisi wa uzazi.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na Nipashe, Dk. Kakumbi amesema changamoto za uzazi zinawahusu wanandoa wote wawili, lakini mara nyingi wanawake hubeba lawama na unyanyapaa katika jamii kwa kuitwa majina kama wagumba au tasa, ilhali vipimo vinaweza kubaini tatizo linatokana na mwanaume.
"Mwanaume anaweza kujisifu kuwa ana uwezo wa kufanya tendo la ndoa mara nne kwa siku, lakini hiyo si dhamana kwamba ana uwezo wa kumpa mwanamke ujauzito. Anaweza kuwa na nguvu za kufanya tendo la ndoa, lakini mbegu zake zikawa hazina uwezo wa kutungisha mimba," amesema.
Ameeleza kuwa uchunguzi wa kitaalamu hubaini changamoto mbalimbali zinazoweza kuathiri uwezo wa mwanaume kupata mtoto, ikiwemo kuwa na idadi ndogo ya mbegu, mbegu kutokuwa na uwezo wa kusafiri vizuri au kuwa na maumbo yasiyo ya kawaida, kama vile kichwa kikubwa kupita kiasi au mikia miwili, hali inayopunguza uwezo wa kutungisha ujauzito.
Dk. Kakumbi amewataka wanaume kuondoa hofu ya kufanyiwa vipimo na badala yake kutafuta huduma za kitabibu mapema ili kubaini chanzo cha tatizo na kuanza matibabu stahiki.
"Hatupigi ramli, tunafanya uchunguzi wa kitaalamu unaotusaidia kubaini chanzo cha tatizo na kuanza matibabu sahihi. Wengi wanaobadili mtindo wa maisha na kufuata ushauri wa wataalamu hupata matokeo mazuri," amesema.
Aidha, amewasihi wanandoa wanaokabiliwa na changamoto ya kupata mtoto kutafuta ushauri wa kitabibu mapema badala ya kulaumiana, akibainisha kuwa maendeleo ya sayansi yameongeza fursa za matibabu ya uzazi saidizi na kuwapa wengi matumaini ya kutimiza ndoto ya kupata watoto.
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED