Chalamila: Wananchi tembeleeni maonesho ya Sabasaba

By Imani Nathaniel , Nipashe
Published at 05:51 PM Jul 07 2026
news
Picha Iman Nathaniel
Chalamila: Wananchi kutembeleeni maonesho ya Sabasaba

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila amewahamasisha wananchi kuendelea kutembelea Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba), akisema maonesho hayo yameendelea kuvutia idadi kubwa ya watu wanaokwenda kujifunza, kununua bidhaa na kupata huduma mbalimbali za kijamii.

Ametoa wito huo leo baada ya kutembelea viwanja hivyo, huku akieleza kuwa uongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam unafarijika kuona mwitikio mkubwa wa wananchi katika maonesho hayo, jambo linaloonesha kuwa yameendelea kuwa na manufaa kwa Watanzania.

Pia amewasilisha salamu za Rais Samia Suluhu Hassan, akisema serikali itaendelea kuyatumia maonyesho hayo kama jukwaa la kuwasiliana na wananchi, pamoja na kuhamasisha biashara, uwekezaji na maendeleo ya uchumi.

“Maonesho ya mwaka huu yanatimiza miaka 50 tangu kuanzishwa kwake na yamewakutanisha zaidi ya kampuni 25 zinazonesha bidhaa, teknolojia na huduma mbalimbali, huku zikiwapa wananchi fursa ya kununua bidhaa kwa bei za punguzo maalumu katika kipindi cha maonesho,” amesema.

Ameongeza kuwa wananchi wanaotembelea Sabasaba wanaweza pia kupata huduma mbalimbali za kijamii, zikiwemo upimaji wa macho, ushauri wa afya na huduma zinazotolewa na wizara pamoja na taasisi mbalimbali za serikali.

Aidha, amewashauri wananchi wenye migogoro ya ardhi kutembelea mabanda ya taasisi zinazoshughulikia sekta hiyo ili kupata ushauri wa kisheria na huduma kutoka kwa wataalamu waliopo katika maonesho hayo.

1
Kutokana na mwitikio mkubwa wa wananchi, Mkuu huyo wa Mkoa amesema kuna umuhimu wa kujadili uwezekano wa kuongeza siku mbili au tatu za maonesho hayo kwa kushirikiana na Wizara ya Viwanda na Biashara pamoja na waandaaji, ili Watanzania wengi zaidi wapate fursa ya kunufaika na huduma zinazotolewa.

Naye, Kamanda wa Polisi Kanda Maalium ya Dar es Salaam, Jumanne Murilo, amewatoa hofu wananchi na kuwataka waendelee kujitokeza kwa wingi kutembelea maonesho hayo, akisisitiza kuwa ulinzi na usalama umeimarishwa katika viwanja vya Sabasaba.

Amesema Jeshi la Polisi limejipanga kikamilifu kupambana na uhalifu katika kipindi chote cha maonesho, hivyo wananchi hawapaswi kuwa na hofu wanapotembelea viwanja hivyo.