AAFP: Maridhiano CCM, ACT yataondoa migogoro ya kisiasa

By Rahma Suleiman , Nipashe
Published at 02:31 PM Jul 08 2026
news
Picha Rahma Suleiman
AAFP: Maridhiano CCM, ACT yataondoa migogoro ya kisiasa

Chama cha Wakulima (AAFP) kimeunga mkono maridhiano kati ya CCM na ACT Wazalendo, kikisema tamko la pamoja litakalotiwa saini litafungua ukurasa mpya wa kuondoa migogoro ya kisiasa na kuimarisha umoja wa Wazanzibari.

Akizungumza na waandishi wa habari katika makao makuu ya chama hicho, leo Mwera, Mwenyekiti wa AAFP, Said Soud, amesema wananchi wamekuwa na kiu ya kuona siasa za maridhiano zinazoweka mbele maslahi ya taifa kuliko tofauti za kisiasa.

“Tamko hili ni muhimu kwa sababu viongozi wetu wazalendo wameamua kutatua changamoto zao wenyewe badala ya kusubiri suluhu kutoka kwa viongozi wa nje,” amesema Said.

Amesema hatua hiyo ni ya kupongezwa kwakuwa inaonesha ukomavu wa kisiasa na inaleta matumaini ya kujenga Zanzibar yenye utulivu, mshikamano na mazingira bora ya maendeleo kwa wananchi wote.

Said amesisitiza kuwa mafanikio ya maridhiano hayo yanapaswa kuungwa mkono na kuwepo kwa katiba itakayobeba na kulinda makubaliano hayo ili yawe na manufaa ya kudumu kwa Wazanzibari.

“Lengo letu ni kuona migogoro ya kisiasa inakuwa historia na wananchi wanaishi kwa amani, wakielekeza nguvu zao katika maendeleo ya Zanzibar,” amesema.

Aidha, ametoa shukrani kwa marais wastaafu Amani Abeid Karume na Dk. Ali Mohamed Shein kwa mchango wao katika kusukuma mbele ajenda ya maridhiano, pamoja na Rais Dk. Hussein Ali Mwinyi na Mwenyekiti wa ACT Wazalendo kwa uamuzi wao wa kufanikisha makubaliano hayo.