Waziri Mkuu UK ajiuzulu, aahidi kugeukia mke, watoto

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 01:04 PM Jun 22 2026
Waziri  Mkuu wa Uingereza, Keir Starmer.
Picha: Mtandao Wetu
Waziri Mkuu wa Uingereza, Keir Starmer.

Waziri Mkuu wa Uingereza, Keir Starmer, ametangaza kujiuzulu wadhifa huo, akisema anaheshimu mawazo ya chama chake cha Labour, baada ya mpinzani wake kuibuka kidedea Ijumaa iliyopita.

Starmer ametangaza uamuzi huo leo Juni 22, 2026 mbele ya waandishi wa habari, huku mrithi wake akitarajiwa kuingia madarakani kabla ya Bunge kurejea mwezi Septemba, hatua itakayofanya Uingereza kupata kiongozi wake wa saba katika kipindi cha miaka 10.

Starmer anajiuzulu wadhifa huo alioutumikia chini ya miaka miwili tangu aliposhinda uchaguzi mkuu kwa kishindo mwaka 2024, kwa ahadi ya kumaliza machafuko ya kisiasa nchini humo.

Amesema mchakato wa kupokea majina ya wagombea wa nafasi yake utaanza Julai 09, huku mpinzani wake, Andy Burnham, akitajwa kuwa mgombea anayeongoza kwa sasa.

“Swali ambalo chama changu kinauliza sasa ni kama mimi ndiye mtu sahihi wa kukiongoza kuelekea uchaguzi mkuu ujao. Nimesikia jibu la wabunge wa chama changu kuhusu swali hilo, na ninalikubali kwa moyo mkunjufu,” amesema Starmer.

Starmer amesema atakiomba chama kuweka ratiba rasmi ya uchaguzi wa uongozi, huku uteuzi wa wagombea ukianza Julai 9. Ataendelea kushika nafasi yake hadi mchakato huo ukamilike na ameahidi kufanya kila awezalo kuhakikisha makabidhiano yanafanyika kwa utaratibu.

Amesema anatarajia kiongozi mpya wa Labour na Waziri Mkuu mpya wawe madarakani ifikapo Septemba wakati Bunge litakaporejea.

Akihitimisha hotuba yake, Starmer alionekana akishindwa kuzuia hisia, machozi yakimlengalenga huku sauti yake ikitetemeka. Amesema baada ya kuondoka katika nafasi kubwa zaidi ya kisiasa nchini Uingereza, atajikita katika jukumu muhimu zaidi maishani mwake – kuwa mume bora kwa mke wake Victoria na baba bora kwa watoto wake.

Starmer anaondoka madarakani baada ya miezi kadhaa ya shinikizo, lililoongezeka zaidi Ijumaa iliyopita baada ya Burnham, Meya wa Greater Manchester, kushinda kwa kishindo uchaguzi mdogo wa ubunge na kurejea Westminster. 

Katika uchaguzi huo alimshinda mgombea wa chama cha Reform UK kinachoongozwa na Nigel Farage, ambacho kimekuwa kikiongoza kura za maoni za kitaifa kwa zaidi ya mwaka mmoja.

Ushindi huo uliwapa matumaini wabunge wa Chama cha Labour kwamba Burnham, mwanasiasa mwenye uzoefu na anayejulikana kwa uwezo wake wa mawasiliano, anaweza kubadili mwelekeo wa chama hicho ambacho kimepoteza uungwaji mkono chini ya Starmer. Ripoti zinasema kwamba umaarufu wa Starmer umeshuka hadi viwango vya chini zaidi kuwahi kushuhudiwa kwa kiongozi yeyote wa Uingereza.

Masoko ya fedha yamepokea tangazo hilo kwa utulivu, huku thamani ya paundi na hati fungani za serikali ya Uingereza zikibaki karibu na viwango vya awali kutokana na matarajio ya wawekezaji kwamba angeondoka madarakani.

Kwa mujibu wa mfumo wa bunge wa Uingereza, kiongozi wa chama chenye wabunge wengi ndiye anayekuwa Waziri Mkuu.

Kwa sasa chama cha Labour ndicho chenye idadi kubwa ya wabunge na mchakato wa kumpata Waziri Mkuu mpya utaanza kwa kuchaguliwa kwa kiongozi mpya wa chama hicho.

Reuters