Kwa miezi kadhaa, matamshi dhidi ya wahamiaji yamekuwa yakiongezeka nchini Afrika Kusini, jambo lililowalazimu wahamiaji kadhaa kuondoka nchini humo wakati Juni 30 ikikaribia, tarehe ambayo wahamiaji wasio na vibali wametakiwa kuondoka katika taifa hilo.
Mwanzoni mwa mwezi Juni, wanaume wawili walitoa kauli ya mwisho kwa mkulima wa Malawi, Kaunga Nyirenda, ambaye anaishi katika vitongoji vya Johannesburg, kuondoka mara moja au kufa.
"Waliniuliza unapanga kuondoka lini nchini tunataka kuiweka sawa nchi yetu, usipoondoka sasa utaondoka ukiwa ndani ya jeneza maana hatuhitaji mgeni yeyote baada ya Juni 30," amesema Nyirenda ambaye ni raia wa Malawi.
Imeelezwa kuwa kauli hizo anzilizoelekezwa kwa Nyirenda zilionyesha kuongezeka kwa jumla kwa hisia za kupinga wahamiaji.
Katika wiki za hivi karibuni, makundi ya waandamanaji na wanaojiita wanamgambo, ambao wanadai maandamano yao ni ya amani, wamefanya maandamano ambayo yameonekana kuibua mashambulizi makali dhidi ya raia wa kigeni, wasio kuwa na vibali au wale wanaoishi kisheria nchini humo.
Wawili hao wanatuhumiwa kuiba kazi za Waafrika Kusini, kufanya uhalifu na kuelemea huduma za umma.
Aidha, imeelezwa kuwa serikali ya Afrika Kusini imefuta kile kinachoitwa "makataa" yaliowekwa na makundi hayo kwa wageni kuondoka nchini, huku hofu ya kuzuka kwa ghasia mwishoni mwa mwezi huu ikiongezeka.
Moja ya makundi hayo, March & March, limetoa wito wa maandamano makubwa kesho ikiwa matakwa yake, ikiwemo kufukuzwa mara moja na kwa wingi kwa wageni wote haramu kwa sasa katika eneo hilo, hayatatekelezwa.
Kabla ya maandamano yaliyopangwa, Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa alionya kwamba serikali "haitavumilia jaribio lolote la kuhatarisha usalama wa taifa, iwe kwa maandamano au vinginevyo."
Amelaani mara kwa mara mashambulizi dhidi ya raia wa kigeni, akisema "hayawakilishi maoni ya raia wa Afrika Kusini wala sera ya serikali yetu." Ramaphosa amesema vikosi vya usalama viko katika hali ya tahadhari kujibu machafuko yoyote.
HOFU YA KIUSALAMA
Kutokana na mvutano unaozidi kuongezeka, polisi wa Afrika Kusini wamefungua uchunguzi kuhusu mauaji ya hivi karibuni ya raia kadhaa wa kigeni.
Polisi wamesema raia wawili wa Msumbiji waliuawa wakati wa ghasia mwishoni mwa mwezi Mei huko Mossel Bay, mji wa pwani katika Rasi ya Magharibi, ambako zaidi ya vibanda 50 katika eneo la vijijini vilichomwa moto.
Msumbiji baadaye ilitangaza vifo vya raia wake watano katika kile ilichokiita "mashambulizi ya chuki dhidi ya wageni."
RFI
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED