Nigeria yalaani raia wake wawili kuuawa

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 12:49 PM Jul 05 2026
Nigeria yalaani raia wake wawili kuuawa
Picha: Mtandao
Nigeria yalaani raia wake wawili kuuawa

Nigeria imelaani madai ya kuuawa kwa raia wake wawili nchini Afrika Kusini na kuitaka serikali ya nchi hiyo, kufanya uchunguzi wa haraka na kuwawajibisha waliohusika.

Katika taarifa iliyotolewa leo, Jumapili, na Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Nigeria, Kimiebi Imomotimi Ebienfa, amesema mmoja wa raia hao anadaiwa kuuawa na maofisa wa Polisi wa Manispaa ya Tshwane mjini Pretoria, Juni 28, 2026.

Nigeria pia imesema raia mwingine aliuawa kwa kupigwa risasi nje ya duka lake mjini Witbank, katika Jimbo la Mpumalanga, na watu wasiojulikana siku hiyo hiyo.

Serikali ya Nigeria imesema ina wasiwasi mkubwa na vifo hivyo, ikidai vinatokea wakati ambapo raia wa kigeni wanazidi kulengwa nchini Afrika Kusini.

Abuja pia ilirejelea kifo cha raia mwingine wa Nigeria aliyedaiwa kuuawa na maafisa wa Polisi wa Manispaa ya Tshwane, Aprili, ikisema hakuna mtu aliyekamatwa kuhusiana na tukio hilo.

Nigeria imezitaka mamlaka za Afrika Kusini kufanya uchunguzi wa haraka kuhusu vifo hivyo na kesi nyingine zinazohusisha raia wake, huku ikisisitiza kwamba watuhumiwa wanapaswa kufikishwa mbele ya sheria bila kuchelewa.

Nigeria imewashauri raia wake waliopo Afrika Kusini kubaki watulivu, kuheshimu sheria za nchi hiyo na kuepuka maeneo yaliyoathiriwa na maandamano dhidi ya wahamiaji.

Nigeria imesema itaendelea kuwahamisha raia wake kutoka Afrika Kusini. 

Zaidi ya raia 700 tayari wamerejeshwa nchini humo kupitia safari nne za ndege, huku safari nyingine mbili zikitarajiwa kufanyika Julai 6 na Julai 9, 2026.

Hadi sasa, mamlaka za Afrika Kusini hazijatoa tamko rasmi kuhusu madai mapya ya Nigeria.

Chanzo: BBC