Iran: Makubaliano sio ushindi kwa Marekani

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 10:47 AM Jun 25 2026
news
Picha Mtandao
Iran: Makubaliano sio ushindi kwa Marekani

Iran imesema kilichothibitika hadi sasa ni kushindwa kwa ubabe wa Washington, huku Shirika la Nguvu za Atomiki Duniani (IAEA) likishikilia kupatiwa fursa ya kuendeleza ukaguzi kwenye vinu vya nyuklia vya Iran.

Mkuu wa timu ya upatanishi ya Iran, Mohammad Bagher Qalibaf, ameyataja makubaliano yanayoendelea sasa kati ya nchi yake na Marekani kuwa ni "tangazo la kushindwa la Washington".

Akizungumza kupitia televisheni ya Iran siku ya jana Qalibaf amesema makubaliano ya Islamadab hayakutokana na shinikizo na vitisho "bali yalikuwa matokeo ya mapambano na mamlaka ya taifa jasiri la Iran."

"Ndio maana makubaliano hayo yamekuwa tangazo la Marekani kushindwa vita," amesema.

Qalibaf, Spika wa Bunge na mwanasiasa mwenye ushawishi na uzoefu mkubwa wa masuala ya kijeshi na kiutawala, amezungumza hayo akiwa ndio kwanza amerejea akitokea nchini Oman, alikokwenda kuzungumzia hatima ya Mlango Bahari wa Hormuz na taifa hilo jirani, ambalo kwa pamoja na Iran, wanamiliki njia hiyo muhimu kwa kupitishia nishati ya mafuta na gesi ulimwenguni. 

Amesema kuanzia sasa ni jukumu la mataifa ya Mashariki ya Kati na Ghuba pekee kuhakikisha usalama wa eneo lao na sio la mgeni yeyote, akimaanisha Marekani na washirika wake wa Magharibi, bila kuwataja kwa majina.

Oman yaruhusu meli kupita

Kwa upande wa Oman imesema itaendelea kuiacha wazi sehemu yake ya Mlango Bahari wa Hormuz ili kuziruhusu meli kupita bila kuzitoza malipo yoyote.

Pia imesema kutokana na ukosefu wa usalama, Muscat imeanzisha njia za muda kwa meli hizo kupita upande wa kaskazini na kusini mwa Mlango Bahari huo.

Iran na Oman zimeanza majadiliano juu ya mustakabali wa usimamizi wa safari na huduma kwenye Mlango Bahari wa Hormuz leo.

Ingawa makubaliano ya sasa kati ya Marekani na Iran yanatowa nafasi kwa meli kupita bila vikwazo kwa muda wa siku 60, mazungumzo ya majirani hao wawili yanadhamiria kupata mpango wa muda mrefu, zikiwemo gharama za usafirishaji, baada ya kipindi hicho kumalizika.

IAEA yataka iruhusiwe kuingia Iran

Katika hatua nyingine, Mkuu wa Shirika la Nguvu za Atomiki la Umoja wa Mataifa (IAEA), Rafael Grossi, amesema kwamba ni haki ya shirika lake kupewa nafasi ya kurejea Iran kuendelea na ukaguzi wa vinu vya nyuklia Iran kufuatia makubaliano kati ya Tehran na Washington.

Akiwa mjini Tokyo, Japan, Grossi amesema mbali na mivutano ya kisiasa za kila upande, makubaliano hayo yanatamka wazi juu ya utekelezwaji wa jukumu hilo.

"Hili limesainiwa kabisa, limekubaliwa hivyo. Kipengele nambari nane cha makubaliano hayo kinasema kwa uwazi kabisa kwamba shughuli za kinyuklia zitakazofanyika kwenye vinu na vifaa kinyuklia zitasimamiwa na IAEA, hilo lipo kwa ufasaha kabisa," amesema Grossi.

Hadi sasa msimamo wa Iran ni kwamba wakati inakubaliana kushirikiana tena na IAEA, bado haiko tayari kuwaruhusu wakaguzi wa shirika hilo kuingia nchini humo hadi baada ya kukamilika kwa mazungumzo na mkataba kamili kupatikana.

DW