Watalii 6,700 watembelea kijiji cha nyuki Singida

By Thobias Mwanakatwe , Nipashe
Published at 06:05 PM Jul 06 2026
Mkurugenzi wa Kijiji cha Nyuki, Philemon Kiemi.
Picha:Mpigapicha Wetu
Mkurugenzi wa Kijiji cha Nyuki, Philemon Kiemi.

Watalii 6,790 kutoka ndani na nje ya Tanzania walitembelea Kijiji cha Nyuki kilichopo Kisaki, Manispaa ya Singida, katika kipindi cha mwaka jana kwa lengo la kujionea vivutio mbalimbali, ikiwamo bustani ya miti ya asili pamoja na bidhaa zinazotokana na nyuki, hususan Vumbi la Singida.

Mkurugenzi wa Kijiji cha Nyuki, Philemon Kiemi, alisema kati ya watalii hao, 1,620 walitoka katika nchi mbalimbali zikiwamo Marekani, Israel, Ujerumani, China, Australia na Poland.

Akizungumza na waandishi wa habari  jana waliotembelea kijiji hicho, Kiemi alisema wageni wengi huvutiwa na uwepo wa miti ya asili inayopatikana kwa wingi mkoani Singida pamoja na vyakula vya asili vinavyotolewa katika kijiji hicho.

Alisema miongoni mwa vyakula vinavyowavutia zaidi watalii ni ugali wa mlenda, ambao wengi wao wamekuwa wakiusifu kutokana na ladha yake ya kipekee.

Kiemi alisema kivutio kingine kikubwa ni Vumbi la Singida, bidhaa inayokusanywa na nyuki kutoka kwenye maua ya miti na mimea inayostawi katika mazingira yasiyo na uchafuzi wa mazingira, jambo linalolifanya kuwa na virutubisho vingi muhimu kwa afya ya binadamu.