Zaidi ya Sh bilioni 21 zimelipwa kwa wakulima wa ufuta mkoani Pwani kupitia minada mitatu ya kwanza ya zao hilo, huku Chama Kikuu cha Ushirika cha CORECU kikieleza kuwa malipo ya mnada wa nne yatafanyika mara tu wanunuzi watakapokamilisha taratibu za malipo.
Akizungumza na waandishi wa habari katika mnada wa nne wa ufuta uliofanyika katika ghala kuu la Kibiti, Meneja wa CORECU Mkoa wa Pwani, Hamis Mantawela, amesema mfumo wa minada umeendelea kuhakikisha wakulima wanalipwa kwa wakati.
"Leo ni mnada wa nne wa ufuta kufanyika mkoani Pwani. Kupitia minada mitatu iliyopita, zaidi ya Sh bilioni 21 zimelipwa kwa wakulima," amesema Mantawela.
Amewashukuru wanunuzi kwa kutekeleza malipo kwa wakati, akieleza kuwa baada ya kupewa ankara (invoice), hulipa ndani ya saa 72, hatua inayorahisisha fedha kuwafikia wakulima mapema.
"Tunawashukuru wanunuzi kwa kulipa kwa wakati. Tunapowapa invoice hulipa ndani ya saa 72, kinachobaki ni fedha hizo kuwafikia wakulima," amesema.
Mantawela amesema CORECU kwa kushirikiana na wadau imehakikisha wakulima wote waliouza mazao katika minada iliyopita wamepokea malipo yao, huku akiahidi kuwa malipo ya mnada wa nne nayo yatafanyika kwa wakati.
Amewahimiza wakulima kuendelea kupeleka ufuta katika vyama vya msingi badala ya kuhifadhi nyumbani, akieleza kuwa upungufu wa mazao kwenye maghala unaweza kuwafanya wanunuzi kuelekeza ununuzi wao katika maeneo mengine, hali inayoweza kushusha ushindani wa bei.
Katika mnada wa nne, jumla ya tani 1,800 za ufuta ziliuzwa, ambapo bei ya juu ilikuwa Sh2,560 kwa kilo na bei ya chini Sh2,310 kwa kilo.
Mantawela amesema bei za ufuta zimeendelea kuwa nzuri katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo. Kwa mujibu wa takwimu hizo, Mkuranga kilo moja iliuzwa kwa wastani wa Sh2,392.50, Kibiti Sh2,399.97, Ikwiriri Sh2,457.42 na Kibaha Sh2,336.44.
Naye mkulima wa Kijiji cha Bungu, Ahmed Juma, ameishukuru Serikali kwa juhudi za kutafuta masoko ya zao la ufuta, lakini ameiomba iendelee kufanya mazungumzo na wanunuzi ili bei iongezeke zaidi.
"Tunashukuru Serikali kwa kututafutia masoko, lakini tunaomba itusaidie kuhakikisha bei ya ufuta inapanda zaidi. Gharama za uzalishaji ni kubwa na wakati mwingine fedha tunazopata haziendani na uwekezaji tulioufanya katika kilimo," amesema.
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED