Serikali imetoa wito kwa wawekezaji kutumia fursa zilizopo katika sekta ya misitu na nyuki kwa kuwekeza zaidi kwenye uongezaji thamani wa mazao yatokanayo na sekta hizo, hatua inayolenga kuongeza thamani ya bidhaa, kukuza ajira na kuchangia ukuaji wa uchumi wa taifa.
Akizungumza katika Banda la Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kwenye Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Hamad Hassan Chande, amesema sekta ya nyuki ina fursa kubwa za kiuchumi kutokana na uzalishaji wa asali na bidhaa nyingine zinazohitajika ndani na nje ya nchi.
Amesema serikali inawahimiza wawekezaji kuwekeza katika uchakataji na uongezaji thamani wa mazao ya misitu na nyuki ili kuongeza ushindani wa bidhaa hizo katika masoko ya ndani na kimataifa.
Aidha, Naibu Waziri huyo amewataka wananchi kujitokeza kuchukua mbegu za miti mbalimbali, hususan miti ya asili ambayo imeanza kupotea, ili zipandwe katika maeneo mbalimbali nchini.
"Tunatoa wito kwa wananchi waje kuona misitu mbalimbali tuliyonayo. Tuna mbegu za miti ya misitu ambayo imeanza kupotea. Waje wazichukue na wazipande katika maeneo yao, na serikali iko tayari kutoa elimu ya uoteshaji wa mbegu na upandaji wa miti," amesema.
Amesema wananchi, hususan wa Dar es Salaam na maeneo mengine nchini, wanapaswa kujenga utamaduni wa kupanda miti katika makazi yao kwa kuwa, mbali na kupendezesha mazingira, miti huzalisha oksijeni na kufyonza hewa ya kaboni dioksidi, hivyo kusaidia kulinda mazingira na afya za wananchi.
"Unapojenga nyumba yako nzuri, panda pia miti. Mbali na kupendezesha mazingira, miti inazalisha oksijeni tunayohitaji na kufyonza kaboni dioksidi, hivyo ina mchango mkubwa katika kuhifadhi mazingira," amesema.
Kadhalika, amesema misitu ina faida nyingi zikiwamo kulinda vyanzo vya maji, kuhifadhi bioanuwai na kuboresha mandhari ya mazingira.
Naibu Waziri huyo amewataka wananchi kutumia fursa ya Maonesho ya Sabasaba kutembelea banda la TFS kwa ajili ya kupata mbegu za miti pamoja na elimu ya upandaji miti na uhifadhi wa misitu.
Vilevile, amewataka wananchi kuacha vitendo vya kuchoma moto misitu, akieleza kuwa moto husababisha uharibifu wa misitu hiyo, kuathiri uchumi wa taifa na kuharibu maisha ya wananchi wanaotegemea rasilimali hizo.
"Kila mmoja awe mzalendo wa kulinda misitu yetu. Unapoichoma misitu, hauharibu mazingira pekee bali pia unaathiri uchumi wa nchi na hata wa kwako mwenyewe," amesema.
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED