PSSSF yawatambua wastaafu 7,881 kutekeleza kaulimbiu ya ‘Tunalipa Jana’

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 05:09 PM Jul 07 2026
PSSSF yawatambua wastaafu 7,881 kutekeleza kaulimbiu ya ‘Tunalipa Jana’
Picha: Mpigapicha Wetu
PSSSF yawatambua wastaafu 7,881 kutekeleza kaulimbiu ya ‘Tunalipa Jana’

Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) umewatambua wanachama 7,881 wanaotarajiwa kustaafu katika mwaka wa fedha 2026/27, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuhakikisha wanapata mafao yao kwa wakati kupitia kaulimbiu ya ‘Tunalipa Jana’.

Hayo yalisemwa na Mkurugenzi wa Uendeshaji wa PSSSF, Hajj Khamisi, alipozungumza katika banda la Mfuko kwenye Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam yanayoendelea katika Viwanja vya Julius Nyerere.

Amesema Mfuko ulianza maandalizi mapema kwa kushirikiana na waajiri ili kuhakikisha mchakato wa ulipaji mafao unakamilika bila ucheleweshaji.

“Tulikwishawasiliana na waajiri tangu mwezi Machi 2026 kwa kuwapatia orodha ya watumishi wanaotarajiwa kustaafu pamoja na tarehe zao za kustaafu,” amesema.

Khamisi amewashukuru waajiri kwa kuendelea kuwasilisha madai ya watumishi kwa wakati, akisema ushirikiano huo unarahisisha Mfuko kuyachakata madai na kuwezesha wastaafu kupata mafao yao kwa wakati.

“Hii itasaidia kutekeleza kaulimbiu yetu ya ‘Tunalipa Jana’ na kuwaletea tabasamu wastaafu wetu,” ameongeza.

Akizungumzia mchango wa teknolojia katika kuboresha huduma, Mkurugenzi wa TEHAMA wa PSSSF, Eric Kato, amesema mifumo ya kidijitali ya Mfuko imeboreshwa kwa kiwango kikubwa, jambo lililorahisisha utoaji wa huduma kwa wanachama.

Amesema kupitia mifumo hiyo, wanachama wanaweza kuwasilisha madai yao wakiwa popote walipo bila kulazimika kusafiri, hatua inayookoa muda na gharama.

“Karibu asilimia 100 ya huduma zetu zinatolewa kupitia mifumo ya mtandao. Hii imepunguza matumizi ya karatasi na kuokoa fedha za Serikali, huku ikiongeza ufanisi wa utoaji wa huduma,” amesema Kato.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Fedha wa PSSSF, Ally Yakuti, amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuwezesha Mfuko kwa kuwasilisha michango ya wanachama kwa wakati.

Amesema hali hiyo imeuwezesha Mfuko kutekeleza wajibu wake wa kulipa mafao ya mkupuo na pensheni za kila mwezi bila kuchelewesha wanachama wanaostaafu.

“Hakuna sababu ya mwanachama kucheleweshewa mafao yake pindi anapotimiza masharti ya kustaafu. Ndiyo maana tunasema ‘Tunalipa Jana’, tukimaanisha mwanachama hapaswi kusubiri haki yake,” amesema Yakuti.

Baadhi ya wastaafu wanaopokea pensheni kupitia PSSSF walithibitisha kupata malipo yao kwa wakati, wakisema mfumo wa Mfuko umeendelea kuimarika.

“Pensheni yangu huwa naipata vizuri tarehe 22, wakati mwingine tarehe 23 au 24. Haijawahi kuchelewa, nashukuru sana,” amesema Margareth Onjari.

Naye Said Mohammed amesema wakati mwingine pensheni huingia mapema kuliko ilivyozoeleka.

“Mwezi uliopita pensheni iliwahi sana. Nafikiri ni kutokana na maendeleo ya teknolojia. Kwa upande wangu sijapata tatizo lolote na PSSSF,” amesema.