Mfumo wa kufuatilia, kudhibiti na kukusanya taarifa za mafuta yanayoingia nchini kwa wakati halisi (Supervisory Control and Data Acquisition - SCADA) umeendelea kuwa nyenzo muhimu katika kuimarisha usimamizi wa mafuta nchini kwa kuongeza uwazi, usahihi wa taarifa na ufanisi katika ushushwaji wa mafuta kutoka bandarini hadi maghala ya kuhifadhia.
Kupitia mfumo huo, Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (PBPA) umefanikiwa kuimarisha udhibiti wa upotevu wa mafuta na kuongeza uhakika wa takwimu zinazotumika katika kufanya maamuzi ya kiutendaji.
Akizungumza jijini Dar es Salaam kwenye Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Sabasaba yanayoendelea jijini Dar es Salaam, Afisa Lojistiki wa Mafuta wa PBPA, Hilda Kowero, alisema mfumo wa SCADA umeleta maboresho makubwa katika usimamizi wa mafuta kwa kuwezesha ufuatiliaji wa shughuli zote muhimu kwa wakati halisi.
Amesema teknolojia hiyo inawawezesha kupata taarifa sahihi kwa wakati kuhusu mwenendo wa mafuta yanayoingia nchini, hivyo kuongeza uwezo wa kufuatilia mnyororo mzima kwa usahihi na kuimarisha uwajibikaji katika sekta ya mafuta.
Kowero ameongeza kuwa pamoja na kuratibu uagizaji wa mafuta kupitia Mfumo wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (Bulk Procurement System - BPS), PBPA ina jukumu la kuhakikisha nchi inakuwa na akiba ya kutosha na upatikanaji wa mafuta unaoaminika wakati wote.
Amesema hatua hiyo inaimarisha usalama wa upatikanaji wa mafuta nchini na kuchochea ufanisi katika sekta ya nishati kwa ujumla.
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED