Thamani ya kulinda watoto wetu, tujifunze na madhila nje mipaka

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 12:19 PM Mar 19 2026
Familia
AI
Familia

Binafsi nikiwa mama na mwananchi, huwa kuna wakati nikitafakari hali ya amani duniani na kinachoendelea, kisha nikigeuza shingo yangu kwa watoto wetu tulio nao, huwa napata simanzi.

Kisa na mkasa hapo, neno amani tulilohubiriwa na waasisi wetu wa nchi, ikidumu leo kila kona katika siasa na mahubiri ya imani, nabaki na tafakari kubwa.

Hapo thamani ya watoto niliyo nayo hapa nchini inapanda maradufu.

Inapotokea tumewanyima malezi na matunzo sahihi, najihisi tunakuwa tumekosea sana, kuanzia kijamii, kiimani hata kisheria na vyovyote vile mtazamo wetu unapoangukia, mtoto huyo ana thamani kubwa.

Hata tukiangukia sheria zetu kitaifa, Sheria ya Mtoto, pia ile ya elimu, hadi inayokabaliana na makosa ya kujamiiana, unakuta ndani yake mtoto analindwa hasa!

Kuanzia hilo hapa nyumbani ninapomwona mtu anakinzana na hayo, hisia zangu zinaniambia ‘anatenda kosa hasa’, sijui hata nisemeje?

Wanasema, kama kwako huoni jaribu kusafiri kwa wenzako kuangalia yanayowakuta. Ukianzia na kwetu, baadhi ya watoto wanaishi kwenye mazingira magumu kutokana na migogoro iliyopo katika familia zao, misuguano baina ya makabila au jamii na kadhalika.

Tukivuka mipaka leo na kukanyaga Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini, kuna vurugu na migogoro ya silaha, ikiithiri pakubwa maisha ya watoto, hata inaiamsha Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) kutoa onyo kuhusiana na hilo.

Mnamo tarehe 6 ya Februari jijini Amman, Jordan, Mkurugenzi wa Kanda wa UNICEF kwa Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini, Edouard Beigbeder, akasema watoto katika eneo hilo wanaendelea kuuawa, kujeruhiwa.

Pia, wanalazimika kuhama makazi yao, wanakamatwa na kuzuiliwa, hata kunyimwa huduma muhimu kama vile afya na elimu, huku migogoro ikiendelea katika nchi kadhaa.

Syria nako, mapigano mapya yamesababisha wastani watu 200,000 kuyahama makazi yao, nusu yao, laki moja ni watoto, kukivuruga huduma zao muhimu. 

UNICEF ikaripoti watoto kadhaa kufariki dunia, kwa ukosefu wa huduma za afya na mahitaji ya majira ya baridi.

Nchini Sudan ilikuwa mwezi Januari 2026 mwaka huu, takribani watoto 20 waliuawa. Pia, mamilioni ya watoto wakahitaji msaada kuokoa maisha yao, njaa ikiwalelea. 

Takribani maeneo 20 mengine yako katika hatari ya kukumbwa na njaa kutokana na migogoro inayozuia usambazaji wa misaada ya kibinadamu.

Nchini Iran matukio ya hivi karibuni yamekuwa na athari kubwa kwa watoto na vijana. Zaidi ya watoto 144 wameripotiwa kuuawa, wengine wengi wakiripotiwa ama kujeruhiwa au kuzuiliwa, hata UNICEF ikaendelea kuishinikiza serikali ya Iran kulinda watoto dhidi ya vurugu.

Katika ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan kule Israel, ongezeko la vurugu limeendelea kudhoofisha usalama wa watoto na kuacha familia katika hofu na wasiwasi wa kudumu. Mfano mwezi Januari, watoto wawili waliuawa na wengine 25 kujeruhiwa.

Nchini Yemen, watoto wanaripotiwa kuendelea kukabiliwa na migogoro mingi katika vita vinavyoendelea, matatizo ya kiuchumi na utapiamlo ulioenea. 

Shirika hilo limezitaka serikali na pande zote zinazohusika katika migogoro kuheshimu wajibu wao chini ya sheria za kimataifa za kibinadamu na haki za binadamu na kuchukua hatua za haraka kukomesha mauaji, majeraha, kukamatwa, kuzuiliwa na kuwatia watoto hofu na majeraha ya kisaikolojia.

 “Watoto wote wanachohitaji zaidi ni amani,” inasema UNICEF.

Timu ya pamoja ya Umoja wa Mataifa ya kutathmini misaada ya kibinadamu ikiongozwa na WHO ilifika katika Hospitali ya Al-Shifa Kaskazini mwa Gaza ili kutathmini hali ilivyo.