SIMULIZI ya maisha ya Rosie Male tuliyochapisha katika toleo letu la jana, si hadithi ya kawaida ya maisha ya mtu mmoja. Ni kioo kinachoakisi dosari nzito ndani ya mfumo wa haki jinai nchini.
Ni simulizi inayoumiza, inayoshtua na inayopaswa kuamsha dhamiri ya taifa kuhusu namna haki inavyotolewa au kunyimwa kwa wananchi wake.
Rosie alikuwa na ndoto ya kuwa mwanasheria. Ndoto halali iliyojengwa juu ya juhudi na matumaini, lakini ilikatizwa ghafla alipokamatwa bila kuelewa kosa lake, kisha baadaye kujikuta akikabiliwa na shtaka la mauaji, hatimaye kuhukumiwa kifo.
Hapa ndipo swali la msingi linapoibuka: mfumo wetu wa haki unamlinda nani na kwa kiwango gani?
Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, kila mtu ana haki ya kusikilizwa kwa haki mbele ya mahakama. Haki hii si mapambo ya kisheria, ni nguzo kuu ya ustaarabu na utawala bora.
Lakini katika safari ya Rosie, haki hii ilionekana kuchelewa na kuchelewa huku kulimgharimu miaka ya ujana wake, amani ya akili na hata uhusiano wa kifamilia.
Kukaa gerezani kwa miaka kadhaa bila uhakika wa hatima yako, ukisubiri hukumu ya kunyongwa, ni adhabu kubwa kisaikolojia, hata kabla ya hukumu yenyewe kutekelezwa. Ni mateso yasiyoonekana lakini yenye athari kubwa.
Zaidi ya hayo, kucheleweshwa kwa nyaraka za kesi na kukosekana kwa msaada wa kisheria kwa wakati kunazua maswali makubwa kuhusu ufanisi na uadilifu wa mifumo ya uchunguzi na uendeshaji kesi.
Ni jambo la kusikitisha kwamba haki ya Rosie ilikuja baada ya juhudi zake binafsi na bahati ya kupata fursa ya kusikilizwa na kiongozi wa juu serikalini. Je, ni wangapi hawapati nafasi hiyo? Je, ni wangapi wanaendelea kuteseka magerezani kwa sababu hawana sauti ya kusikika?
Simulizi hii inapaswa kuwa mwito wa mageuzi ya kina katika mfumo wa haki jinai. Ni lazima tujiulize: je, uchunguzi wa makosa ya jinai unafanyika kwa weledi na haki? Je, watuhumiwa wanapatiwa msaada wa kisheria kwa wakati? Je, ucheleweshaji kesi unadhibitiwa ipasavyo?
Ni wazi kuwa kuna upungufu unaohitaji kushughulikiwa kwa haraka. Serikali, mahakama, vyombo vya uchunguzi na wadau wa haki za binadamu wanapaswa kuimarisha mifumo ya kuhakikisha haki inatolewa kwa wakati na kwa usawa.
Hii ni pamoja na kuongeza idadi ya mawakili wa msaada wa kisheria, kuboresha mifumo ya upatikanaji nyaraka za kesi na kuimarisha uwajibikaji kwa maofisa wanaochelewesha au kukiuka taratibu kama ilivyopendekezwa pia na Tume ya Rais ya Haki Jinai mwaka juzi.
Vilevile, Nipashe tunaamini kuwa ni wakati mwafaka kwa taifa kuendelea kujadili kwa kina adhabu ya kifo. Wakati kuna hoja za kuiunga mkono, simulizi kama ya Rosie zinaonesha hatari iliyopo pale ambapo mfumo unakosea.
Je, tuna uhakika gani kwamba kila anayehukumiwa kifo amepata haki ya kutosha? Hili ni swali linalohitaji mjadala mpana wa kitaifa.
Pamoja na maumivu aliyopitia, Rosie ameonesha uthabiti wa kipekee kwa kugeuza mateso yake kuwa chachu ya kusaidia wengine kupitia taasisi yake.
Huu ni ushahidi kwamba hata katika giza nene, mwanga unaweza kupatikana. Lakini haipaswi kuwa jukumu la waathirika pekee kurekebisha mfumo uliowaumiza.
Kwa ujumla, simulizi ya Rosie ni onyo na somo kwa taifa. Ni wito wa kuhakikisha kuwa haki haitolewi kwa kuchelewa, kwa bahati au kwa upendeleo, bali kwa wakati, kwa usawa na kwa uadilifu.
Taifa linalothamini haki za raia wake ndilo linalojenga msingi imara wa amani, maendeleo na mshikamano wa kijamii.
Tusipuuze kilio hiki. Tusikubali ndoto nyingine kunyongwa kimyakimya. Wakati wa mageuzi ni sasa.
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED