Ardhi ya Z'bar isigeuke uwekezaji wa kusubiri

Nipashe
Published at 02:26 PM May 12 2026
Zanzibar
Picha: Mtandao
Zanzibar

UAMUZI wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) wa kuanza mchakato wa kuvichukua zaidi viwanja 300 vilivyotelekezwa kwa zaidi ya miaka 25 katika maeneo ya Mzuri, Tasani na Kiongoni, Makunduchi, ni hatua inayostahili kuungwa mkono kwa maslahi mapana ya taifa na wananchi wake.

Ardhi ni rasilimali adhimu isiyoongezeka, hivyo haiwezi kuachwa mikononi mwa watu wanaoishikilia bila kuiendeleza huku maelfu ya wananchi wengine wakihangaika kutafuta maeneo ya kujenga makazi yao.

Kwa muda mrefu kumekuwapo tabia ya baadhi ya watu kuomba viwanja vya serikali si kwa dhamira ya kuviendeleza, bali kwa nia ya kuvihifadhi kama vitega uchumi vya baadaye.

Wengine wamekuwa wakisubiri thamani ya ardhi ipande ili wauze kwa faida kubwa, wakati maeneo hayo yakibaki mapori yasiyo na manufaa yoyote kwa jamii.

Hali hii imekuwa ikikwamisha upangaji bora wa miji, kuathiri utoaji huduma za kijamii na kuchelewesha maendeleo ya maeneo mengi ya makazi.

Kauli ya Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Ardhi Zanzibar, Mussa Kombo, kwamba Sheria ya Ardhi Na. 12 ya mwaka 1992 inamtaka mwenye kiwanja kukiendeleza ndani ya miaka miwili tangu kukabidhiwa, inaonesha wazi kuwa serikali haichukui hatua hii kwa pupa wala kwa hisia. Ni utekelezaji sheria iliyopo kwa muda mrefu.

Kinachoshangaza ni kwa nini baadhi ya wamiliki wa viwanja wameamua kupuuza masharti hayo kwa zaidi ya miongo miwili bila kuchukua hatua yoyote ya maendeleo.

Ni jambo lisilokubalika kuona wananchi wakipewa viwanja tangu mwaka 2000, lakini mwaka 2026 bado maeneo hayo hayana hata dalili ya msingi wa nyumba.

Huu si tu uzembe wa wamiliki wa viwanja, bali pia ni dalili ya udhaifu wa mifumo ya ufuatiliaji iliyopaswa kuhakikisha sheria inatekelezwa mapema. Serikali imekiri kuwa hatua hizi zilipaswa kuchukuliwa zamani zaidi.

Hili ni somo muhimu kwa taasisi zote zinazohusika na usimamizi wa ardhi kuwa kuchelewa kuchukua hatua kunazalisha migogoro na kuendeleza matumizi mabaya ya rasilimali za umma.

Hata hivyo, pamoja na kuunga mkono hatua hiyo, Nipashe tunaona ni muhimu serikali ikazingatia misingi ya haki, uwazi na ushirikishwaji katika utekelezaji wake.

Wapo wananchi ambao huenda walishindwa kuendeleza viwanja vyao kutokana na changamoto za kiuchumi, ukosefu wa mitaji au sababu nyingine za msingi.

Serikali inapaswa kuhakikisha kila mhusika anapewa nafasi ya kusikilizwa kabla ya uamuzi wa mwisho kufanyika. Utaratibu wa kutoa notisi uliotajwa na Kamisheni ya Ardhi ni hatua nzuri inayopaswa kuendelezwa kwa haki na uwazi.

Vilevile, serikali inapaswa kuweka mfumo madhubuti wa kuhakikisha viwanja vinavyorejeshwa havigeuki tena kuwa chanzo cha upendeleo, rushwa au ugawaji usiozingatia vigezo vya haki. Wananchi wengi wana uhitaji mkubwa wa maeneo ya makazi, hivyo ugawaji mpya unapaswa kufanyika kwa uwazi na kwa kuzingatia maslahi ya umma.

Kwa upande mwingine, hatua hii inapaswa kuwa fundisho kwa wananchi wote waliopatiwa ardhi ya serikali katika maeneo mbalimbali nchini. Umiliki wa kiwanja si suala la fahari pekee, bali ni wajibu unaoambatana na utekelezaji masharti ya kisheria.

Serikali inapotoa ardhi kwa wananchi, lengo lake ni kuona maendeleo ya makazi, biashara au huduma nyingine yanapatikana kwa manufaa ya jamii nzima.

Zanzibar inaendelea kukua kwa kasi katika sekta za utalii, biashara na huduma za kijamii. Ukuaji huo unahitaji mipango bora ya matumizi ya ardhi ili kuzuia holela, migogoro ya ardhi na uchakavu wa mazingira.

Viwanja vinapobaki bila kuendelezwa kwa robo karne, maana yake ni kwamba maendeleo ya eneo husika nayo yanakwama. Kwa msingi huo, hatua ya serikali ichukuliwe kama mwanzo wa kuimarisha nidhamu ya matumizi ya ardhi Zanzibar.

Sheria lazima iheshimiwe kwa wote bila upendeleo. Ardhi ya umma inapaswa kutumika kwa maendeleo ya wananchi na si kuwa mali ya kuhifadhiwa kwa matarajio ya faida binafsi za baadaye.