Mwaka 1971, nguli wa fasihi ya Kiswahili, Profesa Euphrase Kezilahabi, aliandika riwaya ya Rosa Mistika, kazi iliyotikisa fikra za jamii kwa kuanika dhuluma, ukandamizaji na udhaifu wa mifumo inayomwacha mwanamke peke yake katika mapambano ya maisha.
Leo, zaidi ya nusu karne baadaye, simulizi hiyo si hadithi tu ya kifasihi; imegeuka kuwa taswira halisi ya maisha ya baadhi ya wajane nchini.
Taarifa kutoka Chama cha Wanawake Wajane Tanzania (CCWWT) zinaonesha hali ya kutisha. Wajane wanauawa, wananyanyaswa na wengine kufikia hatua ya kujitoa uhai kutokana na msongo wa mawazo unaotokana na migogoro ya mirathi.
Haya si matukio ya kubuni, bali ni uhalisia unaoendelea kushuhudiwa katika jamii zetu kuanzia Geita hadi Morogoro.
Ni wazi kuwa tatizo hili lina mizizi katika mifumo miwili mikuu; ule wa kijamii unaoendeleza mila kandamizi na ule wa kisheria unaochelewesha haki.
Kesi za mirathi zinazodumu kwa miaka 10 hadi 20 si tu zinachelewesha haki, bali zinaua matumaini ya maisha kwa wanawake wanaobeba mzigo wa familia peke yao. Hapa ndipo tunapaswa kujiuliza: haki inayochelewa ni haki kweli?
Kwa upande mwingine, jamii imeendelea kushuhudia ukatili wa kutisha dhidi ya wajane. Kuuawa kwa kisingizio cha mali ni kielelezo cha kushindwa kwa mifumo ya ulinzi wa raia.
Huu si mgogoro wa kifamilia tena. Ni suala la haki za binadamu linalohitaji msimamo mkali wa dola. Vyombo vya dola vinapaswa kuongeza kasi ya uchunguzi na kuhakikisha wahusika wanawajibishwa ipasavyo ili kutoa funzo kwa wengine.
Hata hivyo, lawama haziishii kwa vyombo vya dola pekee. Jamii nayo ina wajibu wa kujitathmini. Mila na desturi zinazomnyima mwanamke haki ya kumiliki mali au kumweka pembezoni baada ya kifo cha mumewe zinapaswa kupingwa kwa nguvu zote.
Huu ni wakati wa kuachana na mitazamo ya kizamani inayohalalisha dhuluma kwa jina la utamaduni.
Simulizi ya Esther Raphael, mkazi wa Tegeta Wazo, inatoa mwanga katikati ya giza hili. Pamoja na kupitia misukosuko mikubwa kuanzia kifo cha mumewe, kuuzwa kwa mali zote kwa ajili ya matibabu na athari za kiafya za msongo wa mawazo, bado ameendelea kusimama na kulea familia yake.
Huu ni ushahidi kuwa wajane si waathirika tu, bali pia ni mashujaa wa kimyakimya wanaohitaji kuungwa mkono, si kuonewa.
Nipashe tunaona huu ni wakati sasa kwa serikali kuangalia upya mifumo ya usimamizi wa mirathi, kuhakikisha kesi zinamalizika kwa wakati na kwa haki.
Huduma za msaada wa kisheria zinapaswa kupanuliwa, hasa kwa makundi yaliyo hatarini kama wajane.
Vilevile, mifumo ya hifadhi ya jamii na uwezeshaji kiuchumi kwa wajane inapaswa kupewa kipaumbele ili kuwajengea uwezo wa kujitegemea.
Katika ngazi ya kimataifa, Umoja wa Mataifa (UN) ulitambua umuhimu wa kulinda haki za wajane kwa kuanzisha Siku ya Wajane Duniani kila Juni 23.
Hata hivyo, maadhimisho haya hayapaswi kubaki kuwa matamko ya kila mwaka. Yanapaswa kuwa kichocheo cha hatua madhubuti za sera na utekelezaji wake.
Tunapaswa kukiri ukweli mchungu kwamba, kama jamii itaendelea kukaa kimya, basi "Rosa Mistika" itaendelea kuandikwa upya katika maisha halisi ya wanawake wengi. Hili si jambo la kujivunia, bali ni aibu ya kitaifa.
Ni wakati wa kuchukua hatua kwa sababu nyuma ya kila kesi ya mirathi, kuna maisha ya mwanamke, na nyuma ya kila mjane, kuna mustakabali wa taifa.
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED