TFF ifanyie kazi mapungufu upangaji ratiba Ligi Kuu Bara

Nipashe
Published at 12:10 PM Jun 22 2026
TFF ifanyie kazi mapungufu   upangaji ratiba Ligi Kuu Bara
Picha: Maktaba
TFF ifanyie kazi mapungufu upangaji ratiba Ligi Kuu Bara

MPIRA wa miguu ni mchezo pendwa ambao unaunganisha watu, kuchochea uchumi na kuimarisha taswira ya taifa.

Mpira wa miguu ndio mchezo ambao watu wengi wanafuatilia mashindano kuanzia yanapoanza mpaka yanapomalizika na kuonyesha ni namna gani ni mchezo pendwa. 

Kutokana na umuhimu wake ndiyo maana ratiba za mashindano ya ndani zinapaswa kupangwa kwa umakini mkubwa ili kuendana na kalenda za kimataifa, hususan matukio makubwa kama Fainali za Kombe la Dunia. 

Kwa Tanzania, suala la upangaji wa ratiba ya Ligi Kuu Tanzania Bara si jambo la kawaida tena, bali ni hitaji muhimu kwa maendeleo ya mchezo huo.

Katika miaka ya hivi karibuni, kumekuwa na malalamiko kutoka kwa wadau mbalimbali kuhusu msongamano wa ratiba za ligi, michuano ya kimataifa na majukumu ya timu za taifa. 

Hali hiyo imekuwa ikisababisha changamoto kwa klabu, wachezaji, waamuzi na hata mashabiki wenyewe.

Kombe la Dunia ni tukio kubwa zaidi katika soka ulimwenguni, mamilioni ya mashabiki huelekeza macho yao kwenye mashindano hayo, huku vyombo vya habari na wadhamini wakijikita zaidi katika kufuatilia mechi zake. 

Katika mazingira hayo, kuendelea na ratiba za ligi bila kuzingatia tukio hilo kunaweza kupunguza mvuto wa mashindano ya ndani.

Ni muhimu kwa mamlaka zinazosimamia soka nchini kupanga ratiba za ligi kwa kuzingatia kalenda ya Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) na Shirikisho la Soka Afrika (CAF). 

Hii itasaidia kuepuka migongano inayoweza kuathiri ubora wa mashindano na ushiriki wa wadau katika ligi za ndani, hapa TFF kuna la kujifunza katika kutatua mgongano huu.

Wachezaji wengi wangependa kushududia michezo ya Kombe la dunia wakiwa hawana majumu kwenye klabu zao, nikimaanisha kama wangekuwa kipindi cha mapumziko wangekuwa na wasaha mkubwa wa kufuatilia michezo ya Kombe la dunia na kujifunza vitu kutoka uko.

Pia, ratiba iliyopangwa vizuri huwapa makocha muda wa kutosha kuandaa timu zao. Msimu wenye msongamano wa mechi huongeza hatari ya majeraha kwa wachezaji na kupunguza kiwango cha ushindani kutokana na uchovu.

Kwa upande wa mashabiki, ratiba bora huwasaidia kupanga muda wa kufuatilia mechi za ligi na zile za kimataifa bila usumbufu. Mashabiki ndio uti wa mgongo wa mchezo wa soka, hivyo maslahi yao yanapaswa kupewa uzito mkubwa.

Aidha, wadhamini wa ligi hunufaika zaidi pale ratiba inapokuwa wazi na inayotabirika. 

Kampuni nyingi huwekeza fedha nyingi katika soka kwa lengo la kupata mwonekano wa kutosha. 

Ratiba zinazobadilishwa mara kwa mara au kugongana na matukio makubwa zinaweza kupunguza thamani ya uwekezaji wa wadhamini.

Kwa sasa hapa nyumbani Ligi Kuu bado inaendelea huku pia kukiwa na matukio makubwa ya soka duniani, hususaniKombe la dunia na kuwapa wakati mgumu mashabiki kufuatilia nini.

Ligi yenye ratiba nzuri huongeza uaminifu wa wadau kwa waandaaji wake, klabu hupata nafasi ya kupanga safari, mazoezi na bajeti zao mapema bila kukumbwa na mabadiliko yasiyo ya lazima.

Tunaamini, katika mchakato wa bodi ya Ligi kukusanya maoni ya marekebisho ya kanuni za uendeshaji wa ligi, suala la upangaji waratiba linapaswa kuangaliwa kwa uamkaini mkubwa.

Ratiba ya Ligi Kuu iangalie matukio yote makubwa ya soka, lakini pia iendane na ratiba ya Shirikisho la soka Afrika (CAF).