Tanzania tutumie fursa hii ya Miss World 2027

Nipashe
Published at 10:37 AM Apr 27 2026
Tanzania tutumie fursa hii ya Miss World 2027
Picha: Mtandao
Tanzania tutumie fursa hii ya Miss World 2027

TANZANIA itaandika historia yake kwenye ramani ya dunia baada ya kuthibitishwa rasmi kuwa mwenyeji wa mashindano ya 74 ya urembo duniani (Miss World 2027).

Hatua hiyo imekuja baada ya kusainiwa kwa mkataba rasmi wa maandalizi ya mashindano hayo wiki iliyopita, jijini Dar es Salaam, ambapo Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, alisaini kwa niaba ya Serikali.

Hafla hiyo pia ilishuhudiwa na Waziri wa Wizara hiyo, Paul Makonda, ikihitimisha mchakato uliokuwa ukiendelea kwa muda wa maandalizi ya makubaliano kati ya Tanzania na waandaaji wa mashindano hayo ya kimataifa. 

Akizungumza katika hafla hiyo, Makonda alisema hatua hiyo ni ushindi mkubwa kwa Tanzania na ushahidi kuwa nchi imeanza kuchukua nafasi yake katika matukio makubwa ya kimataifa.

Hata sisi tunapongeza hatua hiyo, kwani hii ni heshima kubwa kwa Tanzania, baada ya kufanya kazi kwa muda kuhakikisha tunatimiza vigezo vyote vya waandaaji wa Miss World. 

Na sasa tunajivunia kufikia hatua hii, mashindano haya yatafungua milango mikubwa ya utalii, uwekezaji na kuitangaza Tanzania kimataifa.

Hivyo, tunaamini kwamba, maandalizi haya yatahusisha wadau mbalimbali wa sanaa, utamaduni na sekta binafsi ili kuhakikisha tukio hilo linakuwa la kiwango cha dunia, na pia itakuwa sehemu ya kutumia fursa hiyo kiuchumi. 

Tunasema hivyo kwa sababu, tunaamini ujio wa Miss World 2027 utakuwa ni jukwaa muhimu la kuionesha Tanzania kwa dunia nzima.

Kupata uenyeji wa Miss World si jambo dogo, hii ni fursa ya kipekee ya kuitangaza Tanzania kuanzia vivutio vya utalii, utamaduni wetu hadi ubunifu wa vijana wetu, Dunia itakuja kwetu, na tunapaswa kujiandaa kuitumia vyema nafasi hii.

Hiyo pia itaifanya Tanzania kuwa nchi ya pili barani Afrika kuandaa mashindano hayo makubwa ya urembo, kwani ikumbukwe Afrika Kusini ilishawahi kuyaandaa mashindano hayo.

Hatua hiyo inaendelea kuonesha dhamira ya serikali kuimarisha sekta ya burudani na kuitumia kama nyenzo ya kukuza uchumi, sambamba na jitihada zinazoendelea za kuiweka Tanzania kwenye ramani ya matukio makubwa duniani.

Pia tunaamini huo utakuwa ni msukumo mpya kwa utalii na burudani nchini na itakuwa fursa ya kuwanufaisha wengi, iwe mmoja mmoja au kwa makundi.

Tunafahamu kwamba, mashindano ya Miss World yana mvuto mkubwa kimataifa na huvutia washiriki na watazamaji kutoka mataifa mbalimbali, hali inayotarajiwa kuongeza mapato ya utalii na kukuza ajira.

Tayari Tanzania imeanza kuonesha mwelekeo huo baada ya kufanikisha mashindano ya kitaifa ya Miss World Tanzania 2026, yaliyovutia ushindani mkali na kuibua vipaji vipya katika urembo na utamaduni. 

Sasa tutumie nafasi hii ya kihistoria, kuelekeza nguvu zetu kwenye maandalizi ya kina ya kuhakikisha Tanzania inakuwa mwenyeji bora wa mashindano hayo. 

Kwa sasa, ni wazi Tanzania haiko tena nyuma, bali imeanza kusimama mbele ya jukwaa la dunia.

Kwani hilo ni tukio kubwa linalotarajiwa kuibadilisha taswira ya sekta ya burudani, utalii na utamaduni nchini.