Wanamasumbwi wetu wanabebwa nyumbani?

Nipashe
Published at 11:06 AM May 04 2026
Wanamasumbwi wetu  wanabebwa nyumbani?
Picha: Mtandao
Wanamasumbwi wetu wanabebwa nyumbani?

MWISHONI mwa wiki iliyopita, wadau wa michezo walipata burudani ya pambano la ngumi lililopewa jina la ‘Vita ya Kisasi’, lililofanyika Ubungo, jijini Dar es Salaam.

Pambano hilo liliwakutanisha bondia wa Tanzania, Ibrahim Mafia, dhidi ya Alvin Camique kutoka Ufilipino. Mafia aliibuka mshindi kwa pointi baada ya raundi nane za ushindani mkali.

Ushindi huo ulikuwa na uzito wa kipekee kwa bondia Mafia, kwani ulikuwa ni wa kulipiza kisasi kufuatia kupoteza pambano la awali dhidi ya mpinzani huyo huyo. 

Kwa mantiki hiyo, Mafia aliingia ulingoni akiwa na dhamira ya kurejesha heshima yake na kwa kiasi kikubwa alifanikiwa kufanya hivyo.

Pamoja na ushindi huo, pambano hilo limeacha gumzo kubwa miongoni mwa mashabiki na wadau wa masumbwi. 

Kumekuwa na mjadala mpana, hasa katika mitandao ya kijamii, baadhi ya wachambuzi na mashabiki wakihoji uhalali wa ushindi huo, wakidai kuwa haukuakisi uhalisia wa pambano lilivyoonekana ulingoni.

Hili si jambo jipya katika tasnia ya masumbwi nchini. Kwa muda mrefu sasa, kumekuwa na malalamiko yanayojirudia kuhusu uamuzi wa majaji, ukitiliwa shaka kuwa unapendelea mabondia wa nyumbani. 

Ingawa uzalendo ni jambo jema, katika michezo ya ushindani, haki na uadilifu vinapaswa kuwa juu ya kila kitu.

Tunapaswa kujiuliza kwa kina: Je, tunawajenga mabondia wetu au tunawapotosha? Bondia anayeshinda kwa uamuzi wenye utata akiwa nyumbani anaweza kujijengea imani ya uongo kuhusu uwezo wake. 

Anapokwenda kushindana kimataifa, ambako majaji ni huru na ushindani ni mkali, hukumbana na uhalisia tofauti na mara nyingi kushindwa.

Hali hii inaweza kudhoofisha juhudi zinazofanywa na wadau mbalimbali kuufufua mchezo wa masumbwi nchini. Ni wazi kuwa kwa sasa kuna jitihada kubwa za kuwekeza katika mchezo huu ili kutoa ajira kwa vijana na kuibua vipaji vipya. 

Hata hivyo, mafanikio ya jitihada hizi yatategemea zaidi uadilifu katika usimamizi wa mashindano kuliko wingi wa fedha zinazowekezwa.

Ni muhimu pia kuangalia ujumbe uliotolewa na Mgeni Rasmi, Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Paul Makonda, ambaye alimzawadia bondia aliyepoteza, Alvin Camique, kiasi cha Sh. milioni tano kwa kile alichoeleza kuwa ni burudani ya kiwango cha juu aliyoitoa ulingoni. Kitendo hicho, bila shaka, kilibeba ujumbe mzito kwa wadau wa mchezo huo.

Kwa tafsiri ya wengi, zawadi hiyo inaweza kuonekana kama ishara kwamba licha ya matokeo rasmi, bado kulikuwa na maswali kuhusu nani aliyetoa burudani bora zaidi. Huu ni ujumbe ambao unapaswa kutafakariwa kwa kina, hasa na waamuzi na waandaaji wa mapambano.

Masumbwi ni mchezo unaohitaji nidhamu, uwazi na uaminifu. Historia inaonesha kuwa Tanzania imewahi kuwa na mafanikio makubwa katika mchezo huu, hasa kuanzia miaka ya 1990 hadi katikati ya miaka ya 2000. 

Hata hivyo, kuporomoka kwa viwango kulichangiwa na sababu mbalimbali, ukiwamo udhaifu wa mifumo ya usimamizi.

Leo, tunapojaribu kuufufua mchezo huu, hatuna budi kujifunza kutokana na makosa ya nyuma. Ni lazima tuhakikishe kuwa kila pambano linaendeshwa kwa haki, majaji wanatoa uamuzi kwa kuzingatia uhalisia wa pambano, na si kwa misingi ya upendeleo.

Kwa kufanya hivyo, tutawajenga mabondia wenye uwezo wa kweli, watakaoweza kushindana na kuleta heshima kwa taifa katika majukwaa ya kimataifa. 

Vinginevyo, tutaendelea kujidanganya na kuurudisha mchezo huu katika dimbwi la kushuka kwa viwango.

Wito wetu kwa wadau wote; waandaaji, majaji, viongozi wa michezo na hata mashabiki ni kuhakikisha wanalinda uadilifu wa mchezo huu. Masumbwi yana nafasi kubwa ya kuleta ajira, kujenga vipaji na kuitangaza Tanzania kimataifa, lakini yote haya yatawezekana tu kama haki itatendeka.

Ni wakati sasa wa kujisahihisha. Tuchague kuwa wakweli badala ya wabebaji. Kwa kufanya hivyo, tutakuwa tunaupambania mustakabali wa masumbwi ya Tanzania kwa vitendo, si kwa maneno.