Hongera Serengeti Boys kufuzu Kombe la Dunia U-17

By Mhariri Mtendaji , Nipashe
Published at 10:58 AM May 18 2026
Hongera Serengeti Boys  kufuzu Kombe la Dunia U-17
Picha: Mtandao
Hongera Serengeti Boys kufuzu Kombe la Dunia U-17

TANZANIA imeendelea kupeperusha vyema bendera yake kimataifa katika mashindano ya dunia baada ya jana, Timu ya Taifa ya Vijana ya umri chini ya miaka 17 maarufu Serengeti Boys kukata tiketi ya kushiriki fainali zijazo za za Kombe la Dunia U-17.

Serengeti Boys imepata tiketi ya kushiriki fainali hizo kwa mara ya kwanza, lakini ikiwa ni mwendelezo mzuri wa utawala wa Rais wa sasa wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Wallace Karia, ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya CAF.

Tanzania imekuwa nchi ya kwanza kukata tiketi ya kushiriki fainali hizo za Kombe la Dunia zitakazofanyika baadaye mwaka huu huko huko Morocco huku Afrika ikitarajiwa kutoa  wawakilishi 10.

Mafanikio hayo yamekuja zikiwa zimepita siku nane tangu dada zao, Timu ya Taifa ya Wanawake wa umri chini ya miaka 20 (Tanzanite Queens), kukata tiketi ya kushiriki fainali za dunia (FIFA Women U-20), zitakazofanyika kuanzia Septemba 5, mwaka huu nchini Poland.

Huu umekuwa ni mwendelezo mzuri kwa timu za Tanzania katika mashindano ya FIFA ambayo yamekuwa yakihusisha zaidi timu za vijana, hili sasa liwe ‘deni’ kwa wakubwa (Taifa Stars), ambao mwakani watakuwa wenyeji wa michuano ya Kombe la Mataifa Afrika (AFCON 2027).

Serengeti Boys imekata tiketi baada ya kupata ushindi wa pili katika mashindano ya Kombe la Mataifa Afrika (AFCON U-17), yanayoendelea huko Morocco, ikiwafunga Msumbiji mabao 2-0 na jana ikiwachapa Angola magoli 3-0.

Ushindi wa mechi hizo mbili, umewapa Serengeti Boys tiketi ya kusonga mbele ikiwa na mechi moja mkononi (dhidi ya Mali), lakini pia ikisubiri kuungana na timu nyingine kutoka Kundi C ambayo itacheza hatua ya robo fainali ya michuano hiyo.

Tunapenda kuchukua nafasi hii kuipongeza TFF, benchi la ufundi na wachezaji kwa juhudi ambazo wameziweka katika kuwaandaa wachezaji hao.

Taarifa kutoka ndani ya shirikisho hilo zinasema, matunda ya kikosi hicho yanatokana na uwekezaji wa muda mrefu, wachezaji wakikaa pamoja kwa muda wa miaka mitatu sasa, isipokuwa nyota wawili  ambao waliitwa kuongeza nguvu siku chache kuelekea fainali hizo.

Siku zote tunafahamu, kuwekeza katika vijana kunalipa, leo hii tunashuhudia Tanzania ikianza ‘kuzoea’ kupeleka timu zake katika mashindano ya FIFA, ilianza mwaka 2022 kwa Serengeti Girls kufuzu fainali za dunia, ikitolewa kwenye hatua ya robo fainali.

Kufuzu ni jambo moja, na kufanya vyema katika michuano mbalimbali ya kimataifa ndio ‘ndoto’ kubwa inayosubiriwa na mashabiki wa soka wa hapa nchini, ambao kwa muda mrefu walikuwa watazamaji kwenye majukwaa ya kimataifa.

Kama ilivyo na changamoto katika kupata udhamini kwenye Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania na Timu za Taifa za wanawake, Serengeti Boys pia ni timu ambayo haina wadhamini, na ili kufikia malengo, inahitaji fedha na vifaa mbalimbali.

Taasisi na makampuni mbalimbali ya ndani na nje, huu ndio wakati wa kujitokeza kusaidia timu hizi ambazo jukumu  lake kubwa ni kupeperusha bendera ya nchi vyema, ili kufikia hayo, fedha zinahitajika.

Watanzania sasa wanataka kuona wawakilishi wetu (Serengeti Boys na Tanzanite Queens), wanaenda kuweka rekodi mpya na ili kufikia malengo hayo, ni lazima timu hizi zipate maandalizi bora na yanayofanana na michuano wanayokwenda kushindana.

Ni timu ya pili ambayo imefuzu michuano mikubwa ikiwa chini ya kocha mzalendo, tuendelee pia kuwaamini makocha wetu kwa kuwawezesha kama vile tunavyowapa dhamana walimu kutoka nje ya Tanzania.

Idara ya ufundi ya TFF inatakiwa kuzitafutia timu hizi mbili michezo ya kirafiki ya kimataifa na timu ambazo zimewazidi viwango kwa ajili ya kuwapa mazoezi sahihi, hili linawezekana endapo mikakati ya mapema itafanyiwa kazi.

Dunia ya sasa haipendezi kuona wawakilishi wetu wanaenda kushiriki fainali hizo za juu kwa kucheza mechi za kirafiki na timu za wakubwa au jinsia tofauti, hapa tutakuwa tunafanya maandalizi ya zimamoto, tutatakiwa tuwatendee haki kwa kuwaandaa katika ubora unaostahili.

Hakuna kisichowezekana, kufuzu ni jambo la kwanza, na kufanya vyema katika mashindano ndio kiu ya Watanzania kwa sasa baada ya kuwa wasindikizaji kwa muda mrefu kwenye michuano ya kimataifa.

Hongera sana Serengeti Boys. Hongera sana Tanzania.