MKASA wa Rehema Ndoje, mwanamke aliyekaa gerezani kwa miaka 26 akisubiri haki baada ya faili la kesi yake kupotea, ni simulizi inayotikisa dhamira ya taifa kuhusu namna mfumo wa haki unavyoweza kumuumiza mwananchi asiye na sauti.
Ingawa Mahakama ya Rufani hatimaye ilimwachia huru Februari mwaka huu, ukweli unabaki kuwa hakuna hukumu inayoweza kurudisha ujana, utu na miaka aliyopoteza akiwa gerezani.
Rehema aliingia gerezani mwaka 1999 akiwa na umri wa miaka 21 baada ya kushtakiwa kwa kumuua mtoto wake wa miezi minane. Mwaka 2007 alihukumiwa kunyongwa hadi kufa, lakini akakata rufani.
Badala ya kupata haki kwa wakati, alikaa karibu miaka 19 akisubiri rufani yake isikilizwe huku nyaraka muhimu za kesi zikidaiwa kupotea.
Tukio hili linaibua maswali kuhusu uwajibikaji ndani ya mfumo wa utoaji haki. Ibara ya 13(6)(a) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 inatoa haki ya kusikilizwa kwa usawa mbele ya sheria.
Vilevile, kifungu cha 359(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai kinampa mshtakiwa haki ya kukata rufani dhidi ya hukumu asiyoridhika nayo. Hata hivyo, haki hiyo haina maana ikiwa mchakato wake utachukua robo karne kutokana na uzembe wa kiutawala.
Ni wazi kuwa kuchelewa kwa haki ni aina nyingine ya adhabu. Rehema hakuteseka kwa sababu ya kifungo pekee, bali kwa sintofahamu ya hatima yake.
Alishuhudia wafungwa wengine wakisikilizwa rufani na kuondoka, huku yeye akiendelea kuhamishwa magereza tofauti bila majibu. Hali hiyo si tu ukiukwaji haki za binadamu, bali pia inavunja misingi ya utu na imani kwa taasisi za sheria.
Kwa miaka ya karibuni, Tanzania imeendelea kufanya maboresho katika sekta ya sheria yakiwamo matumizi ya mifumo ya kidijitali mahakamani.
Hata hivyo, simulizi ya Rehema inaonesha bado kuna mianya mikubwa ya kiutendaji inayoweza kuwaangamiza wananchi wasio na msaada wa kisheria au uwezo wa kufuatilia haki zao.
Jambo lingine linalopaswa kuangaliwa kwa kina ni mjadala kuhusu adhabu ya kifo. Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimeeleza kuwa adhabu hiyo ni ya kikatili na haiendani na misingi ya haki za binadamu.
Umoja wa Afrika (AU) kupitia Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Mataifa, pamoja na taasisi za kimataifa kama Umoja wa Mataifa, zimeendelea kuzihamasisha nchi wanachama kupunguza au kuondoa adhabu ya kifo kwa kuzingatia utu wa binadamu na uwezekano wa makosa ya kimahakama.
Kesi ya Rehema inaonesha hatari ya mfumo unapokosea. Ikiwa angeuawa kabla ya rufani yake kusikilizwa, nani angerudisha maisha yake?
Hili ni somo kwa mamlaka za sheria, mahakama na magereza kuhakikisha mifumo ya uhifadhi wa kumbukumbu inakuwa salama, ya kisasa na yenye uwajibikaji.
Vilevile, kuna umuhimu wa kufanya mapitio ya haraka ya wafungwa wote ambao rufani zao zimekwama kwa sababu za kiutawala.
Taifa haliwezi kujivunia mfumo wa sheria ikiwa bado kuna watu wanaonyimwa haki kwa sababu ya faili kupotea au uzembe wa watendaji.
Kwa upande mwingine, jamii nayo ina wajibu wa kuwapa nafasi mpya waliotoka magerezani. Rehema ametoka gerezani akiwa mtu tofauti, mwenye majeraha ya mwili na akili, lakini pia akiwa na funzo kubwa kuhusu uvumilivu na maisha.
Nipashe tunaamini kuwa simulizi hii ni kengele ya mageuzi. Haki isipochelewa, ndipo sheria huaminika. Lakini haki inapocheleweshwa kwa miaka 26, taifa lote linapaswa kujiuliza: ni wangapi wengine bado wanasubiri kusikilizwa?
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED