Watu wasioona wasiachwe nyuma usalama barabarani

Nipashe
Published at 02:00 PM May 22 2026
Watu wasioona wasiachwe   nyuma usalama barabarani
Picha:Mtandaoni
Watu wasioona wasiachwe nyuma usalama barabarani

CHANGAMOTO zinazowakabili watu wenye ulemavu wa macho katika matumizi ya barabara si suala dogo la kijamii, bali ni mtihani mkubwa wa utekelezaji haki za binadamu na wajibu wa dola katika kulinda usalama wa raia wake wote.

Kauli zilizotolewa na wanachama wa Jumuiya ya Wasioona Tanzania (TAB) katika semina iliyoandaliwa na Taasisi ya Mpango wa Usalama Barabarani (TARSI) jijini Dar es Salaam zinafungua ukurasa muhimu wa mjadala kuhusu namna ambavyo jamii na mifumo yetu ya usafiri imeendelea kuwaacha nyuma watu wenye mahitaji maalumu.

Kwa muda mrefu, mijadala kuhusu usalama barabarani imekuwa ikijikita zaidi kwa madereva, waendesha pikipiki na watembea kwa miguu kwa ujumla, huku makundi maalumu kama watu wasioona yakipewa nafasi ndogo sana. 

Ukweli ni kwamba mazingira ya barabara nchini hayajajengwa kwa mtazamo wa ujumuishi. Kukosekana kwa alama za sauti kwenye taa za barabarani, njia maalumu za waenda kwa miguu wasioona, pamoja na elimu hafifu kwa watumiaji wengine wa barabara kuhusu matumizi ya fimbo nyeupe, kunawaweka watu hawa katika mazingira ya hatari kila siku.

Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 inalinda haki ya usawa na utu kwa kila raia bila ubaguzi. Ibara ya 11 inaelekeza serikali kuweka mazingira yatakayowezesha wananchi wote kupata ustawi na msaada unaostahili. 

Hata hivyo, haki hizi haziwezi kuwa na maana kama kundi la watu wenye ulemavu wa macho linaendelea kushindwa kuvuka barabara salama au kutumia usafiri wa umma kwa heshima na uhuru.

Sheria ya Watu wenye Ulemavu ya mwaka 2010 nayo inaweka wajibu kwa mamlaka kuhakikisha miundombinu, huduma za usafiri na taarifa vinapatikana kwa urahisi kwa watu wenye ulemavu. Lakini uhalisia unaonekana kuwa tofauti. 

Kauli ya Mlezi wa TAB, James Shimwenye kwamba baadhi ya madereva hushindwa kusimama vizuri vituoni ni ushahidi kuwa bado kuna pengo kubwa kati ya sheria na utekelezaji wake. Hili si jambo la kupuuzwa, kwa sababu uzembe huo unaweza kusababisha majeraha au hata vifo.

Kimataifa, Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizoridhia Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Haki za Watu Wenye Ulemavu (CRPD), unaotaka mataifa kuhakikisha mazingira salama, jumuishi na yanayowezesha ushiriki kamili wa watu wenye ulemavu katika maisha ya kijamii na kiuchumi. 

Mkataba huo unasisitiza pia haki ya watu wenye ulemavu kupata uhuru wa kutembea na kutumia huduma za usafiri bila vikwazo. Kwa mantiki hiyo, suala la usalama wa watu wasioona barabarani si hisani, bali ni haki ya msingi inayopaswa kuheshimiwa.

Katika ngazi ya kikanda, Mkataba wa Afrika kuhusu Haki za Binadamu na Watu pamoja na Itifaki zake umeendelea kuhimiza nchi wanachama kuweka sera na mifumo inayolinda makundi yaliyo hatarini. 

Hivyo basi, Tanzania ina wajibu wa kuhakikisha maendeleo ya miundombinu yanakwenda sambamba na mahitaji ya watu wenye ulemavu.

Ni jambo la kutia moyo kuona TARSI na Jeshi la Polisi kupitia Kikosi cha Usalama Barabarani wanaendelea kutoa elimu kwa umma. Hata hivyo, Nipashe tunaamini elimu pekee haitoshi bila uwekezaji wa makusudi katika miundombinu rafiki. 

Barabara nyingi nchini zimejengwa bila kuzingatia mahitaji ya watu wasioona. Vivuko vya waenda kwa miguu havina alama za sauti, baadhi ya njia zimejaa vizuizi visivyoonekana kirahisi, huku vituo vya mabasi vikikosa mpangilio unaowasaidia watu wenye ulemavu wa macho.

Serikali, halmashauri, wahandisi wa barabara na sekta ya usafiri kwa ujumla wanapaswa kutambua kuwa maendeleo hayapimwi kwa ukubwa wa barabara pekee, bali kwa uwezo wa kila mwananchi kuzitumia kwa usalama.

Vilevile, elimu kuhusu kuheshimu watu wenye ulemavu inapaswa kuanzia shuleni hadi katika mafunzo ya udereva ili kujenga jamii yenye uelewa na utu.

Taifa lisipochukua hatua madhubuti leo, watu wenye ulemavu wa macho wataendelea kuishi katika mazingira ya hofu na kutengwa. 

Tanzania yenye usawa ni ile inayomfanya kila raia, awe anaona au haoni, kujisikia salama na kuthaminiwa anapotumia barabara na huduma za umma.