Morocco: Tutajikita kuwa mwenyeji Kombe la Dunia sio barani Afrika

By Mwandishi Wetu , Nipashe Jumapili
Published at 12:11 PM Jun 14 2026
Wachezaji wa Morocco
Picha: Mtandao
Wachezaji wa Morocco

MOROCCO imetangaza kuwa haitawasilisha tena maombi ya kuandaa mashindano ya soka ya Afrika kwa sasa, badala yake ikielekeza juhudi zake katika maandalizi ya matukio makubwa ya soka duniani yanayotarajiwa kufanyika katika miaka ijayo.

Akizungumza kwenye jukwaa la Al Jazeera 360, Rais wa Royal Moroccan Football Federation, Fouzi Lekjaa, amesema kuwa azma ya Morocco ya kuandaa mashindano katika siku zijazo itajikita kwenye michuano ya FIFA, ikiwamo Kombe la Dunia na Kombe la Dunia la Klabu, badala ya mashindano ya bara la Afrika.

“Morocco haitawasilisha tena maombi ya kuandaa mashindano yoyote ya Afrika. Mataifa mengine yakitaka kuyaandaa, yako huru kufanya hivyo,” amesema Lekjaa.

Morocco itakuwa mwenyeji mwenza wa Kombe la Dunia la 2030 pamoja na Spain na Portugal, hatua itakayoifanya kuwa taifa la kwanza la Afrika Kaskazini kuandaa mashindano hayo makubwa ya soka duniani.

Hata hivyo, viongozi wa soka nchini humo wanaamini kuwa maandalizi ya mashindano hayo makubwa ya kimataifa yanahitaji umakini na rasilimali nyingi ili kuhakikisha yanafanyika kwa mafanikio.

Tangazo hilo linaashiria mabadiliko makubwa kwa Morocco, taifa ambalo limekuwa miongoni mwa waandaaji wakuu wa mashindano ya soka barani Afrika katika miaka ya karibuni.

Morocco iliandaa kwa mafanikio 2025 Africa Cup of Nations, baada ya kutunukiwa uenyeji na Shirikisho La Soka Barani Afrika CAF.

Chanzo: BBC