Mwanafunzi apoteza uhai akizama baharini

By Baraka Jamali , Nipashe Jumapili
Published at 04:37 PM Jul 05 2026
Timu ya ukoaji ilipofika eneo hilo
Picha" Baraka Jamali
Timu ya ukoaji ilipofika eneo hilo

MRISHO Hassani Nagwenya (13), mkazi wa Mtaa wa Boma, Kata ya Magengeni, Tarafa ya Mikindani, Manispaa ya Mtwara-Mikindani, amefariki dunia, baada ya kuzama baharini.

Tukio hilo ni baada ya ajali ya mtumbwi iliyotokea Julai 4, 2026, katika eneo la Pemba Mvita, Kata ya Naumbu, Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara.

Marehemu alikuwa mwanafunzi wa Kidato cha Kwanza katika Shule ya Sekondari Mikindani. 

Kwa mujibu wa ndugu wa marehemu, Mrisho alikuwa ameongozana na wenzake wawili kwenda baharini kutafuta mazao ya baharini aina ya kumbwa. 

Baada ya kushindwa kupata, walielekea Pemba Mvita kutafuta matunda ya kunazi.

Walipomaliza shughuli hiyo, walianza safari ya kurejea nyumbani kwa kutumia mtumbwi, lakini upepo mkali uliuzamisha mtumbwi huo na kusababisha Mrisho kuzama, huku wenzake wakinusurika.

"Nilipokea taarifa za ajali hiyo majira ya saa 1:00 usiku baada ya kurejea kutoka shambani. Wananchi waliinza kumtafuta mtoto huyo usiku bila mafanikio na asubuhi kwa kushirikiana na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji tuliendelea na operesheni hadi mwili wake ulipopatikana," amesema Mwenyekiti wa Mtaa wa Mnaida, Ismail Mohamedi.

Maofisa walisema hawakufanikiwa kumwokoa
Ofisa Operesheni wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Mtwara, Mrakibu Msaidizi, Ambrosi Ndunguru, amesema mwili wa marehemu ulipatikana katika pwani ya Pemba, Kata ya Naumbu, baada ya juhudi za pamoja kati ya askari wa zimamoto na wananchi wa vijiji vya ukanda wa Bahari ya Hindi.

"Tunatoa wito kwa wazazi na walezi kuwafuatilia kwa karibu watoto wao, wajue wanapokwenda na shughuli wanazofanya, ili kupunguza matukio ya ajali na kurahisisha utoaji wa msaada wa haraka pale yanapotokea," amesema Ndunguru.