‘Gen Z’ wafikiwa, kupata makazi za bei nafuu

By Pilly Kigome , Nipashe Jumapili
Published at 04:47 PM Jul 05 2026
‘Gen Z’ wafikiwa, kupata makazi za bei nafuu
Picha: Pilly Kigome
‘Gen Z’ wafikiwa, kupata makazi za bei nafuu

KATIKA kutekeleza na kuendana na kasi ya Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, kundi la vija maarufu ‘Gen Z’, wamepata fursa ya kujengewa nyumba za makazi za gharama nafuu, kwa lengo la kuwawezesha wajipange taratibu kupata makazi yao ya kudumu.

Akizungumza na Nipashe Digital jijini Dar es Salaam, leo, Julai 5, 2026, Ofisa Uhusiano wa Wakala wa Majengo Tanzania(TBA), Renatus Sona amebainisha kuwa mpango huo umekuja kwaajili ya kuwawezesha vijana kupata nyumba za bei nafuu, ili kujipanga kiuchumi na kupata makazi yao bora.

Amesema kundi hilo la vijana ni kundi muhimu nchini ambalo ndio nguvu kazi ya taifa kutokana na takwimu inaonesha idadi kubwa ya watu nchini linatoka kwenye kundi hilo, hivyo mpango huo utawawezesha kujipanga na kuwaandaa waweze kujijenga taratibu taratibu.

Amefafanua mradi huo wa nyumba za bei nafuu wameanza kwa Mkoa wa Dar es Salaam katika mradi utakaoitwa Temeke Kota na kufuatiwa na mkoa wa Dodoma na kuenea nchi nzima.

"Hizi nyumba ni mpango mkakati wa kuendana na Dira 2050 kila mtu ana haki ya kuishi kwenye makazi bora na nyumba hizi zitawafanya waweze kupata makazi yao ya kudumu kwakuwa watakuwa wanalipa pango kwa bei nafuu sana, ili waweze kujitafuta kama vijana" amefafanua Sona

Pia amefafanua tayari TBA wameshaainisha maeneo 149 yaliyoiva mikoa yote Tanzania Bara kwaajili ya kutaendeleza kwa njia ya ubia.

Amewaita na kuwakaribisha wawekezaji wa sekta binafsi na taasisi za kifedha kushirikiana katika miradi ya ujenzi wa majumba ya serikali na makazi na kuwakaribisha wananchi kutembelea TBA kupata elimu ya ujenzi wa nyumba bora za makazi.