TANZANIA na Angola, zimesema kuna haja ya kuugeuza uhusiano mzuri wa miaka mingi walionao kuuweka katika matendo katika kushirikiana kwenye biashara na uwekezaji, ili kuzalisha ajira nakuchochea ukuaji wa uchumi kwa nchi hizo mbili.
Akizungumza katika mkutano wa Mamlaka ya Uwekezaji na Kanda Maalum za Kiuchumi Tanzania (TISEZA) wa siku ya Angola kwenye viwanja vya Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (DITF), maarufu Sabsaba, Balozi wa Angola nchini Tanzania, Domingos De Almeida Da Silva Coelho;
Amesema nchi hizo zina historia ya muda mrefu ya ushirikiano, lakini sasa kuna haja ya kuugeuza urafiki huo kuwa matokeo halisi ya kiuchumi.
Mkutano huo, uliokuwa sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Angola katika maonesho hayo, uliwakutanisha viongozi wa serikali, wanadiplomasia na wadau wa biashara kutoka nchi hizo, kwa lengo la kujadili namna ya kupanua biashara, uwekezaji na ushirikiano wa viwanda.
Kwa mujibu wa Balozi huyo, majukwaa ya kimataifa kama maonesho ya Sabasaba yana mchango mkubwa katika kuwaunganisha wawekezaji na kufungua fursa mpya za biashara.
âHaya si maonesho ya bidhaa pekee, bali ni jukwaa la kujenga madaraja ya kudumu ya kiuchumi kati ya mataifa yetu mawili,â amesema.
Ofisa Mwandamizi wa Uwekezaji wa TISEZA, Vedasto Kagombora, amesema Tanzania imeendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji kupitia mageuzi ya sera na mifumo ya udhibiti, ili kuvutia na kuhifadhi wawekezaji wa ndani na wa kimataifa.
Amesema serikali imeweka mfumo thabiti na unaotabirika wa uwekezaji unaolenga kuongeza ushindani na kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha uwekezaji katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Kagombora amesema, ipo fursa kubwa ya kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Angola katika sekta za kilimo, nishati, usafirishaji na viwanda.
Kiongozi huyo wa TISEZA anasema ushiriki wake katika mkutano huo, ni sehemu ya jitihada za kuendelea kuitangaza Tanzania kama kitovu cha ushindani wa uwekezaji na kuimarisha ushirikiano wa kimataifa unaochochea ukuaji jumuishi na endelevu wa uchumi.
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED