WAZIRI wa Afya, Mohamed Mchengerwa ametoa wito wa ushirikiano katika utafiti ugonjwa wa Kifuakikuu (TB), kati ya Tanzania na China, ili kuukabili katika kipindi kifupi tofauti na hali ilivyo sasa.
Mchengerwa ametoa wito huo leo katika Kituo cha âShanghai Sci-Tech Inno Center for Infection & Immunityâ kilichopo Shanghai, nchini China.
Mchengerwa ambaye ameongoza timu ya wataalam kutoka Tanzania na Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Dawa na Vifaatiba, ametembelea maabara ya kituo hicho na kijionea vifaa vya kisasa vya uchunguzi wa magonjwa mbalimbali.
Amependekeza kuanzisha ushirikiano rasmi kati ya kituo hicho cha Shanghai na Hospitali ya Kibong'oto ambayo ameielezea kuwa ni taasisi ya kihistoria inayojihusisha na matibabu na utafiti wa TB nchini, kwa mafanikio makubwa.
"Hospitali ya Kibong'oto mkoa wa Kilimanjaro ilianzishwa mwaka 1926 kama sanatorium ya kifua kikuu. Baada ya muda, ilibadilika kutoka kituo cha matibabu hadi hospitali ya rufani ya kitaifa ya kisasa, na tangu 2006 imekuwa kituo cha kitaifa cha Tanzania cha kifua kikuu sugu,â amesema Mchengerwa
Amependekeza hospitali ya Kibong'oto kuweka nyaraka zake yenye zaidi ya miaka 100 katika mfumo wa kidijitali na kuzichambua kisayansi, ili kufungua njia mpya za kuelewa usugu wa dawa na mabadiliko ya magonjwa.
Ameyataja baadhi ya maeneo muhimu ya ushirikiano kuwa ni pamoja na utafiti wa TB sugu ya dawa, unaolenga epidemiolojia ya molekuli na uchunguzi wa haraka unaofaa mazingira halisi ya kliniki.
Pia amesisitiza kuwa miundombinu itakayojengwa kupitia ushirikiano huu inaweza kuwa msingi wa kukabiliana na magonjwa mapya ya milipuko katika siku zijazo, akisema mchanganyiko wa uzoefu wa kliniki wa Tanzania na uwezo wa utafiti wa China utaimarisha maandalizi ya kimataifa dhidi ya magonjwa yanayoibuka.
Ametoa wito wa moja kwa moja kwa Mkurugenzi Zhang na wenzake Shanghai kuhamia kutoka majadiliano kwenda makubaliano rasmi na utekelezaji akiona ushirikiano huo kama daraja la muda mrefu kati ya uzoefu wa kitabibu Afrika Mashariki na ubunifu wa China.
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED