Katika jitihada za kudumisha umoja na mshikamano miongoni mwa wananchi, Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga, imeandika historia kwa kufanikisha tamasha la amani na maendeleo, lenye lengo kuimarisha umoja kwa wananchi wilayani humo.
Tamasha hilo limefanyika jana katika shule ya Msingi Buduhe, wilayani humo.
Mgeni Rasmi katika tamasha hilo Mbunge wa Jimbo la Kishapu, Lucy Mayenga, amesema hilo ni jukwaa muhimu la kuwakutanisha wananchi wa rika na makundi mbalimbali bila kujali tofauti zao za kijamii au kisiasa, likilenga kuimarisha mshikamano, amani na kuchochea maendeleo ya wilaya.
“Nawapongeza sana wananchi wa Kishapu kwa kujitokeza kwa wingi kwenye tamasha hili, ambalo litaimarisha umoja wetu, mshikamano na kuishi kwa upendo, sababu amani ndiyo msingi wa maendeleo hivyo tuendelee kuilinda na kudumisha amani ya nchi yetu,” amesema Mayenga.
Amesema michezo na burudani husaidia kuondoa tofauti miongoni mwa jamii na kujenga urafiki, hali inayochochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Baadhi ya wananchi walioshiriki tamasha hilo, akiwamo Pili Mazoya, amesema limeweza kuwakutanisha watu mbalimbali na kuimarisha mshikamano na kufurahi kwa pamoja kupitia burudani ya michezo mbalimbali.
Michezo, iliyochezwa kwenye tamasha hilo ni mpira wa miguu, pete, michezo ya asili kama bao, drafti, karata, kufukuza kuku, kuvuta kamba, na mbio za baiskeli.
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED