Winga wa Arsenal, Max Dowman, mwenye umri wa miaka 16, ameweka rekodi mpya ya kuwa mfungaji mwenye umri mdogo zaidi kwenye historia ya Ligi Kuu England, EPL, kwa bao la kushangaza la dakika ya mwisho katika ushindi wa timu yake wa 2-0 dhidi ya Everton, juzi.
Dowman, alikokota mpira kutoka nusu ya uwanja, akawapiga chenga wachezaji wawili wa Everton na kukimbia nao hadi golini na kufunga kirahisi, huku kipa wa Everton, Jordan Pickford akiwa haypo langoni baada ya kwenda mbele kusaidia mashambulizi kwenye kona.
Dowman, akiwa na umri wa miaka 16 na siku 73 - alikuwa akicheza mechi yake ya tatu ya Ligi Kuu England.
Alivunja rekodi ya mchezaji wa zamani wa Everton, James Vaughan, ambaye alikuwa na umri wa miaka 16 na siku 270 alipofunga dhidi ya Crystal Palace mwaka 2005.
"Ilikuwa wakati wa ajabu," alisema kocha wa Arsenal, Mikel Arteta katika mkutano wake na waandishi wa habari, baada ya mchezo huo
"Tulizungumza kabla ya mchezo kuwa ushindi ndio muhimu kwetu. Na kwa juhudi, ubora, na kujitolea kwa wachezaji tuliweza kushinda. Na kisha ikaishia kwa njia ambayo labda hakuna hata mmoja wetu aliyetarajia.
"Na ilikuwa moja ya nyakati bora zaidi ambazo tuliishi pamoja hapa kwenye uwanja wa Emirates.”
Lakini hakucheza mechi ya Ligi Kuu England tangu Septemba, kabla Arteta hajamtumia ‘dogo’ huyo dakika ya 74 Jumamosi huku mchezo bado ukiwa hauna bao.
"Labda kichwani mwangu nilikuwa na hisia ya kuchanganyikiwa,"alisema Arteta kuhusu uamuzi wa kumuingiza Dowman.
"Alikuwa akifanya mazoezi katika siku chache zilizopita, na nilikuwa na hisia ya kuchanganyikiwa kwamba ilikuwa wakati mzuri kwake.
Arteta alisema ujumbe wake kwa Dowman ulikuwa rahisi.
"Nilisema hizi ni nyakati za msimu ambapo jambo maalum lazima litokee, na anajua ana uwezo, ambao lazima nimpe fursa na ataitimiza."
"Nadhani aliunda nguvu tofauti uwanjani," ameongeza Arteta.
"Sio bao pekee alilofunga. Nadhani alibadilisha mchezo. Kila wakati alipopata mpira, alifanya mambo yatokee. Ilionekana kama tulikuwa tishio zaidi.”
Ushindi huo umeiweka Arsenal kileleni mwa msimamo wa kwa tofauti ya 9 dhidi ya Manchester City iliyo nafasi ya pili.
Chanzo: ESPN
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED