Vijana Uchumi Challenge kupewa fursa

By Julieth Mkireri , Nipashe Jumapili
Published at 04:46 PM Jun 28 2026
Vijana Uchumi Challenge kupewa fursa
Picha: Julieth Mkireri
Vijana Uchumi Challenge kupewa fursa

Serikali imesema itaendelea kuwafuatilia vijana 100 walioshiriki katika shindano la Vijana Uchumi Challenge kuona mawazo yao yanafanyiwa kazi na fursa zao haziishii kwenye mafaili pekee.

Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Maendeleo ya Vijana Jenifa Omolo, ameyaeleza hayo jana, mjini Kibaha mkoani Pwani, wakati akifunga kambi ya vijana hao iliyofanyika katika Shule ya Uongozi Mwalimu Nyerere.

Amesema utatengenezwa mfumo ambao Vijana hao watajisajili wote na watakuwa wanafuatiliwa huku akiwasisitiza majaji kuwa karibu na kundi hilo.

Omolo amesema mawazo ya vijana 7852 yalipokelewa na Kamati ya Kitaifa ya Vijana Uchumi Challenge baada ya kuyachuja walipata mawazo 100 na kukutana na vijana hao kwa lengo la kuwapa ujuzi na kuchuja kupata kumi watakaoshiriki katika kilele cha shindano hilo Julai 6.

Amesema Shindano la Vijana Uchumi Challenge ni shindano na jukwaa la kuibua fikra za Vijana, kulea ubunifu, kujenga ujasiri na kuonyesha kwamba vijana wan nafasi kubwa ya kutengeneza suluhisho la kiuchumi.

"Hii ni sehemu ya dhamira ya Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuhakikisha vijana wanashirikishwa kikamilifu katika ujenzi wa Uchumi wa Taifa," amesema.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Vijana Uchumi Challenge, Joseph Malekela, amesema vijana 100 walioshiriki kambi hiyo watatambulishwa kwa viongozi na taasisi za kifedha ili waendeleze mawazo yao kwenye maeneo yao.

Akizungumza kwa niaba ya vanilla wengine Raiyan Juma ameishukuru serikali kwa kuwakutanisha huku wakiomba mawazo yao kutumika katika sekta mbalimbali.

Julai 6, mwaka huu, itakuwa kilele cha shindano hilo ambapo vijana 10 kati ya 100 waliokuwa kwenye kambi hiyo watqkutanishwa na Rais na Mshindi wa kwanza atapatiwa Sh. million 50.

Imeandikwa na Julieth Mkireri, Pwani