Waziri Mkuu, Dk. Mwigulu Nchemba, amewataka watanzania kuendelea kushirikiana katika kulinda amani na usalama wa nchi kwa kutopuuzia viashiria vinavyoweza kuhatarisha utulivu wa Taifa, akisisitiza kuwa ulinzi wa nchi ni jukumu la kila mwananchi.
Akizungumza leo, Juni 28, 2026 katika ibada maalumu ya kilele cha harambee ya nne ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kati, Usharika wa Amani mjini Singida, Dk. Mwigulu amesema watanzania wanapaswa kuwa macho na kushirikiana kulinda amani ambayo imeendelea kuwa msingi wa maendeleo ya taifa.
"Tuendelee kuhimizana kuhusu suala la ulinzi wa Taifa letu. Ulinzi wa Taifa letu ni wa kila Mtanzania na amani yetu ni ya kila Mtanzania," amesema.
Ameongeza kuwa kwa sasa si wakati wa kupuuza dalili zozote zinazoweza kusababisha uvunjifu wa amani kwa kuwa kufanya hivyo kunaweza kuleta athari kubwa kwa taifa.
"Sasa hivi hatupaswi kupuuzia viashiria vya uvunjifu wa amani hapa nchini. Hatutakiwi kuvipuuza kwa sababu vimetuachia doa," amesisitiza.
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED