Wanachama 40, wamo viongozi waihama CUF

By Rahma Suleiman , Nipashe Jumapili
Published at 05:50 PM Jun 28 2026
Wanachama kwenye mkutano
Picha: Rahma Suleiman
Wanachama kwenye mkutano

Wimbi la viongozi na wanachama wa Chama cha Wananchi (CUF) kujiondoa ndani ya chama hicho limeendelea kushika kasi baada ya wanachama 40, wakiwemo viongozi 15 wa ngazi mbalimbali, kutangaza kuachana na chama wakidai kimepoteza mwelekeo kutokana na migogoro ya ndani na ukiukwaji wa katiba yake.

Viongozi hao, wanaojumuisha makatibu wa wilaya, makatibu wa majimbo na wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa kutoka Zanzibar, walitangaza uamuzi huo mbele ya waandishi wa habari, wakisema wamefikia hatua hiyo baada ya kukosa imani na uongozi wa sasa wa chama.

Akizungumza kwa niaba yao, Mwenyekiti wa kikao hicho, Omar Muhammed Hassan, ambaye pia alikuwa Katibu wa Wilaya ya Kaskazini B, amesema CUF kimekuwa kikikabiliwa na migogoro ya muda mrefu iliyoshindwa kupatiwa ufumbuzi, hali iliyowavunja moyo viongozi na wanachama wengi.

Amesema mbali na migogoro hiyo, viongozi hao wanapinga namna Kamati Tendaji ya chama inavyoendesha shughuli zake, wakidai kuwa baadhi ya maamuzi muhimu, ikiwemo mkutano wa viongozi wakuu, yalifanyika bila kuzingatia katiba na taratibu za chama.

Halima Omar, aliyekuwa Katibu wa Wilaya ya Magharib B Unguja, amesema uchaguzi wa ndani wa chama haukuwa wa haki kwa kuwa makatibu wa wilaya hawakushirikishwa, huku akieleza kuwa hakuna utaratibu unaowapa wanachama nafasi ya kuwasilisha malalamiko yao na kusikilizwa.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CUF Wilaya ya Kaskazini A, Vuai Kona Haji, amesema walikuwa na ndoto ya kuona chama kinakuwa mbadala wa uongozi wa nchi, lakini migogoro ya ndani, ubinafsi na kukosekana kwa mshikamano kumezima matumaini hayo.

"Tulijiunga na CUF tukiwa na matumaini ya kujenga chama chenye uwezo wa kushika dola, lakini leo tumebaini chama kimeelemewa na migogoro, ubinafsi na viongozi wasiozingatia katiba. Hatuna tena imani na mwelekeo wa chama," alisema Vuai.

Viongozi hao wamesitiza kuwa uamuzi wao si wa hasira bali umetokana na tathmini ya muda mrefu kuhusu hali ya chama, wakiahidi kutoa msimamo wao kuhusu hatua za kisiasa watakazofuata katika siku zijazo.