LEO ni Siku ya Baba Duniani. Wataalamu wa maendeleo ya watoto na mashirika ya kimataifa wametoa wito kwa jamii kutambua kwamba nafasi ya baba katika familia haipaswi kuishia kwenye jukumu la kutafuta kipato pekee.
Badala yake wanasema, inapaswa kujumuisha ushiriki wao wa karibu katika malezi, elimu na ustawi wa watoto.
Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF), baba ni miongoni mwa rasilimali muhimu zaidi katika maendeleo ya mtoto, lakini bado mchango wao haujatumika ipasavyo katika jamii nyingi duniani.
Shirika hilo linaeleza kuwa watoto wanaopata muda wa kutosha kutoka kwa baba zao huonyesha maendeleo mazuri zaidi katika kujifunza, afya ya akili, kujiamini na uwezo wa kujenga mahusiano wanapokuwa watu wazima.
UNICEF inaeleza kuwa siku 1,000 za kwanza tangu mtoto azaliwe ndizo zinazochangia kwa kiwango kikubwa ukuaji wa ubongo na maendeleo ya baadaye ya mtoto.
Katika kipindi hicho, uwapo wa baba kupitia mazungumzo, michezo, kusoma vitabu pamoja na kushiriki shughuli za kila siku husaidia kuongeza uwezo wa mtoto kujifunza na kukuza hisia za usalama na upendo.
Pamoja na umuhimu huo, takwimu zinaonesha bado kuna changamoto kubwa duniani.
Utafiti uliohusisha nchi 74 ulibaini kuwa zaidi ya asilimia 55 ya watoto wenye umri wa miaka mitatu hadi minne hawashiriki michezo wala shughuli za kujifunza pamoja na baba zao.
UNICEF inakadiria kuwa hali hiyo inawaathiri takribani watoto milioni 40 duniani, jambo linalopunguza fursa za watoto wengi kupata malezi yenye ushiriki wa wazazi wote wawili.
Katika bara la Afrika, wataalamu wa maendeleo ya jamii wanasema bado kuna mtazamo unaowapa baba jukumu la kuwa watoa mahitaji ya kifedha huku malezi ya kila siku yakibaki zaidi kwa mama.
Ingawa mchango wa kiuchumi wa baba ni muhimu, tafiti mbalimbali zinaonesha kuwa watoto hunufaika zaidi pale baba wanaposhiriki moja kwa moja katika maisha yao ya kila siku, ikiwa ni pamoja na kuwasaidia masomo, kucheza nao, kuwapa ushauri na kuwajengea maadili.
Wataalamu wanaeleza kuwa ushiriki wa baba pia huchangia kupunguza changamoto za kitabia kwa watoto, kuongeza ufaulu shuleni na kuboresha afya ya akili.
Watoto wanaokua katika mazingira yenye ushirikiano mzuri kati ya baba na mama huwa na uwezekano mkubwa wa kuwa watu wazima wenye uwezo mzuri wa kufanya maamuzi na kujenga mahusiano imara katika jamii.
Maadhimisho ya Siku ya Baba, pia yanatoa nafasi ya kutafakari nafasi ya wazazi wote wawili katika malezi ya watoto.
Ingawa mara nyingi mjadala huibuka kuhusu nani ana mchango mkubwa zaidi kati ya baba na mama, wataalamu wanasisitiza kuwa hakuna anayepaswa kuonekana kuwa muhimu kuliko mwingine. Kila mzazi ana nafasi yake ya kipekee ambayo haiwezi kuchukua nafasi ya mwenzake.
Kwa mujibu wa UNICEF, watoto wanaostawi zaidi ni wale wanaolelewa katika mazingira yenye upendo, ushirikiano na ushiriki wa wazazi wote wawili.
Shirika hilo linaendelea kuzihimiza serikali, waajiri na jamii kuweka mazingira yanayowezesha baba kutumia muda mwingi zaidi na familia zao kupitia sera rafiki za uzazi, likizo za malezi na mazingira bora ya kazi.
Kwa mujibu wa tovuti ya Statisha, idadi ya kaya zinazoongozwa na wanawake nchini Tanzania imeendelea kuongezeka.
Kati ya mwaka 2017 na 2018, asilimia 28 ya kaya zote ziliongozwa na wanawake, ikiwa ni kiwango cha juu zaidi kuwahi kurekodiwa.
Hali hiyo ni ongezeko kutoka asilimia 25 iliyorekodiwa kati ya mwaka 2007 na 2012.
Hata hivyo, wataalamu wanaeleza kuwa kaya zinazoongozwa na wanawake hazimaanishi zote ni za kina mama wanaolea watoto peke yao (single mothers), kwani baadhi ni za wajane, wanawake waliotengana na wenza wao, au familia ambazo wanawake ndio viongozi wa kaya kwa sababu mbalimbali.
Siku ya Baba ilianza kuadhimishwa mwaka 1910 nchini Marekani kupitia juhudi za Sonora Smart Dodd aliyetamani kumuenzi baba yake, William Jackson Smart, aliyewalea watoto sita peke yake baada ya kufiwa na mke wake.
Baadaye, mwaka 1972, maadhimisho hayo yalitambuliwa rasmi nchini Marekani na sasa huadhimishwa katika mataifa mengi duniani kwa tarehe tofauti.
Wakati dunia ikiendelea kusherehekea siku hii, ujumbe mkubwa unaotolewa na wataalamu ni kwamba mtoto hahitaji mzazi mmoja pekee, bali anahitaji upendo, malezi na ushiriki wa wazazi wote wawili.
Siku ya Baba isiwe tu ya kutoa pongezi, bali iwe fursa ya kuhamasisha baba kushiriki kikamilifu katika kujenga familia imara na kizazi chenye afya, maadili na uwezo wa kuchangia maendeleo ya jamii.
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED