Ofisa Kilimo na wengine wanne kizimbani tuhuma uhujumu uchumi

By Mwandishi Wetu , Nipashe Jumapili
Published at 01:36 PM Jun 21 2026
Watano hao wakiwa kizimbani
Picha: Friday Simbaya
Watano hao wakiwa kizimbani

WATU watano, akiwamo Ofisa Kilimo wa Kijiji, wamefikishwa mahakamani mkoani Iringa wakikabiliwa na mashtaka ya uhujumu uchumi yanayohusiana na madai ya kuuza ardhi kinyume cha sheria.

Washtakiwa hao ni Amini Mwakisambwe, anayedaiwa kuwa Afisa Kilimo wa Kijiji cha Mboliboli, ambaye wakati wa tukio alikuwa akikaimu nafasi ya Mtendaji wa Kijiji, pamoja na Festo Kizumbe, Katalay Mgomboleni, Abdallah Nguswa na Augustino Mkomola.

Watuhumiwa hao walifikishwa mahakamani na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Iringa katika Kesi ya Uhujumu Uchumi Namba ECO 13895/2026.

Upande wa mashtaka ulidai kuwa washtakiwa walipata fedha kwa njia isiyo halali kupitia uuzaji wa kiwanja kinachodaiwa kumilikiwa na Sinzo Masanja kwa mwekezaji Furahini Vahaye.

Aidha, ilidaiwa kuwa Mwakisambwe, akiwa Kaimu Mtendaji wa Kijiji cha Mboliboli, alithibitisha na kuruhusu nyaraka zilizohusiana na mauziano hayo ya ardhi kinyume cha taratibu za kisheria, huku ikidaiwa kuwa ardhi husika haikuwa mali halali ya waliouza.

Kesi hiyo ilisikilizwa mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Honorious Kando, upande wa mashtaka uliongozwa na Wakili wa Serikali Salumu Bhoki akisaidiwa na Lisa Kasongwa.

Akiwasilisha maelezo ya awali ya kesi hiyo, Bhoki alidai kuwa makosa hayo yalitendwa kati ya Februari 1, 2023 na Machi 30, 2023.

Washtakiwa wote watano walikana mashtaka yaliyokuwa yakiwakabili baada ya kusomewa mahakamani na baadaye walipatiwa dhamana.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Julai 17, 2026, itakapotajwa tena mahakamani na upande wa mashtaka unatarajiwa kuwasilisha hoja za awali za kesi hiyo.