Kamati Maalum CHADEMA iliyoketi Z’bar yaja na matano

By Mwandishi Wetu , Nipashe Jumapili
Published at 06:57 PM Jun 14 2026
Bendera ya CHADEMA
Picha: Mtandao
Bendera ya CHADEMA

KAMATI Maalum ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimeazimia maazimo matano, ikiwamo hatua za kuchukua kutokana na hali ya kisiasa nchini.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Makamo Mwenyekiti wa CHADEMA Zanzibar, Said Mzee Said, kikao kilichokaa Juni 7, mwaka 2026, kilipokea na kujadili taarifa mbalimbali kuhusu hali ya kisiasa, kijamii na kiuchumi nchini pamoja na masuala ya ujenzi na uimarishaji wa chama.

Alisema kikao kimeona kuna haja ya kupatikana Katiba Mpya, kutokana na hali ya kisiasa nchini.

“Kamati Maalum imejadili kwa kina hali ya kisiasa nchini na kubaini kuwa changamoto nyingi 
zinazoendelea kuikabili Zanzibar na Tanzania, ikiwamo migogoro ya uchaguzi.

“Matumizi makubwa ya madaraka ya Rais, ukosefu wa uwajibikaji wa taasisi za umma na kuendelea kwa malalamiko kuhusu haki za kiraia na kisiasa, zinatokana na mapungufu ya mfumo wa kikatiba uliopo ambao tumeurithi kwenye ukiritimba wa chama kimoja cha siasa.

“Kutokana na hali hiyo, Kamati Maalum imesisitiza ulazima wa kuanza mchakato wa kuandikwa kwa Katiba Mpya ya wananchi itakayojengwa juu ya misingi ya demokrasia, uwajibikaji, usawa na utawala wa sheria.” 

Amesma Kamati Maalum imeagiza Sekretarieti ya Kamati Maalum kuanza mara moja mchakato wa kuunda Kamati Maalum ya Wataalamu na Wadau ambayo itashirikiana na makundi mbalimbali ya wananchi, asasi za kiraia, vyama vya siasa, taasisi za kitaaluma na viongozi wa dini, ili kufanya uchambuzi wa kina na kutoa mapendekezo ya hatua stahiki za kufanikisha 
upatikanaji wa Katiba Mpya.

“Katiba hiyo inapaswa kuhakikisha kuwa Zanzibar inapata Tume Huru ya Uchaguzi yenye mamlaka kamili ya kusimamia uchaguzi bila kuingiliwa na Serikali au chama chochote cha siasa.

“Uteuzi wa Makamishna wa Tume ya Uchaguzi unafanyika kupitia mchakato huru, shirikishi na wa uwazi. Matokeo ya uchaguzi yanaweza kuhojiwa na kupingwa Mahakamani ili kuhakikisha haki na uadilifu wa uchaguzi.

“Mamlaka na nguvu za Rais zinawekewa mipaka na mifumo madhubuti ya uwajibikaji. Vyombo vya ulinzi na usalama vinafanya kazi zake kwa mujibu wa Katiba na sheria bila kuhusishwa na shughuli za kisiasa.”

Amesema kamati hiyo imazimia wananchi wanakuwa mamlaka kuu ya nchi na hakuna mtu, taasisi au chombo chochote kilicho juu ya Katiba na sheria.

Ameeleza suala lingine lililoazimiwa ni kuhusu kupanda kwa gharama za maisha na mfumuko wa bei na kwamba Kamati Maalum, imepokea taarifa ya Sekretarieti kuhusu hali ya uchumi na mwenendo wa 
maisha ya wananchi nchini. 

Pia amesema Kamati imeeleza wasiwasi mkubwa kuhusu kuendelea kupanda kwa gharama za maisha, ongezeko la bei za bidhaa muhimu, gharama za usafiri, huduma za kijamii pamoja na kupungua kwa uwezo wa wananchi kumudu mahitaji yao ya msingi.

“Kamati imeitaka Serikali kuchukua hatua za haraka na madhubuti za kupunguza mfumuko wa bei, kuimarisha uzalishaji wa ndani, kupunguza kodi zinazoongeza gharama kwa 
wananchi na kuweka mazingira bora ya biashara yatakayochochea ukuaji wa uchumi na ajira.

Amesema suala la tatu katika maazimio ni tathmini ya Bajeti ya Serikali ya Zanzibar 2026/2027, Kamati Maalum ikijadili Bajeti ya Serikali ya Zanzibar kwa mwaka wa fedha 2026/2027 iliyowasilishwa katika Baraza la Wawakilishi na kubaini mapungufu mbalimbali yanayoathiri matarajio ya maendeleo ya wananchi.

Pia amesema Kamati imebaini kuwa bajeti hiyo haijatoa majibu ya kutosha kwa changamoto za msingi zinazowakabili wananchi, hasa kupanda kwa gharama za maisha, ukosefu wa ajira kwa vijana na cangamoto za sekta za kilimo, uvuvi na biashara ndogo ndogo.

“Kuongezeka kwa deni la umma bila maelezo ya kutosha kuhusu manufaa yake kwa wananchi, kutengwa kwa fedha zisizotosheleza katika sekta muhimu za afya, elimu na uwezeshaji wa vijana na wanawake.

“Kutokuwapo kwa mikakati madhubuti ya kuongeza uzalishaji wa ndani na kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje. Kamati imeitaka Serikali kuwasilisha mpango wa wazi wa kuimarisha uchumi wa wananchi na kuhakikisha matumizi ya fedha za umma yanazingatia uwajibikaji, ufanisi na matokeo yanayoonekana kwa wananchi.”

Ameongeza kwamba kuhusu uamuzi wa mwanachama Said Issa Mohamed, Kamati Maalum imepokea taarifa kutoka Kanda ya Pemba kuhusu hatua ya kumvua uanachama aliyekuwa Makamo Mwenyekiti wa CHADEMA Zanzibar,Said Issa 
Mohamed, na baada ya kupitia taarifa, vielelezo na taratibu zote zilizotumika, Kamati Maalum imeridhika kuwa hatua zilizochukuliwa zilizingatia Katiba, Kanuni na taratibu za chama. 

“Hivyo Kamati Maalum imejiridhisha kuwa Ndugu Said Issa Mohamed amepoteza sifa za kuendelea kuwa mwanachama wa CHADEMA na imeunga mkono uamuzi huo.”

Suala la tano amesema ni kuhusu kupitishwa kwa Mpango Mkakati na Mpango Kazi Kamati Maalum imepokea Ripoti ya Kitaalam kuhusu Mpango Mkakati na Mpango Kazi wa CHADEMA Zanzibar kwa kipindi cha mwaka 2026 - 2031.

Amesema baada ya kujadili kwa kina, Kamati Maalum imeridhia na kupitisha rasmi Mpango Mkakati na Mpango Kazi huo kwa ajili ya utekelezaji. Kamati imeelekeza viongozi na watendaji wote wa chama kuhakikisha mipango hiyo inatekelezwa kwa ufanisi, ili kuimarisha chama, kuongeza ushiriki wa wananchi katika shughuli za kisiasa na kuimarisha harakati za demokrasia, uwajibikaji na maendeleo ya wananchi.

“Kamati Maalum inatoa wito kwa wananchi wote wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla kuendelea kushiriki kikamilifu katika mijadala ya kitaifa kuhusu mustakabali wa nchi yetu, hususan masuala ya Katiba Mpya, utawala bora, haki za kiraia, maendeleo ya uchumi na 
uimarishaji wa demokrasia.

“CHADEMA itaendelea kusimama pamoja na wananchi katika kupigania haki, usawa, uwajibikaji wa viongozi na maendeleo endelevu ya taifa letu.”