JAMII imeshauriwa kuwa makini na watu wanaotoa ushauri wa kisaikolojia kupitia mitandao ya kijamii bila kuwa na sifa stahiki, kwakuwa ushauri usio sahihi unaweza kuongeza matatizo ya akili, badala ya kuyatatua.
Mkuu wa Chuo cha Ustawi wa Jamii, Dk. Joyce Nyoni, amesema kuongezeka kwa watu wanaojitambulisha kama washauri wa kisaikolojia bila taaluma husika ni changamoto isiyopaswa kufumbiwa macho, kutokana na athari zinazoweza kujitokeza kwa wanaotafuta msaada.
Akizungumza katika Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea jijini Dodoma, Dk. Nyoni amesema, chuo hicho kinaendelea kuandaa wataalamu wenye sifa katika fani ya saikolojia, ili kuhakikisha huduma za ushauri zinatolewa kwa viwango vinavyokubalika kitaaluma.
"Katika mitandao wapo watu wengi wanaotoa mafunzo na ushauri, lakini wakati mwingine wanachokisema si sahihi. Ndiyo maana sisi tumejikita katika kuandaa wataalamu wenye umahiri wa kutoa huduma za ushauri wa kisaikolojia," amesema.
Amesema pamoja na kutoa huduma za udahili kwa wanaotaka kujiunga na masomo, chuo hicho pia kimeanzisha kituo maalumu katika maonesho hayo kwa ajili ya kutoa huduma za msaada wa kisaikolojia kwa wananchi na watumishi wanaohitaji ushauri wa kitaalamu.
Amesema hicho kinatoa mafunzo mbalimbali kuanzia ngazi ya cheti hadi shahada za uzamili katika fani za maendeleo ya jamii, usimamizi wa rasilimali watu, malezi na makuzi ya awali ya mtoto pamoja na saikolojia.
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED