Wasanii kunufaika na wanaotumia nyimbo zao sehemu za starehe

By Halfani Chusi , Nipashe Jumapili
Published at 09:01 AM Apr 27 2026
Wasanii sasa kunufaika na wanaotumia nyimbo zao sehemu za starehe
PICHA: Halfan Chusi
Wasanii sasa kunufaika na wanaotumia nyimbo zao sehemu za starehe

Ofisi ya Hakimiliki Tanzania (COSOTA) imewakutanisha wadau kutoka sekta ya usafirishaji, utangazaji, kumbi za starehe, hoteli, na maeneo mengine ya biashara ili kujadiliana kwa pamoja namna bora ya utekelezaji wa kanuni za ukusanyaji wa mirabaha kwa mujibu wa sheria chini ya Kampuni zenye leseniza kukusanya na kugawa mirabaha nchini.

Mkutano huo ulifanyika juzi Jijini Dar es salaam, kwa lengo la kujadili na kuona namna mwanamziki husika anaweza kunufaika wimbo wake ukipigwa katika maeneo hayo.

Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu na Msimamizi wa Hakimiliki chama hicho, Naomi Mangure amesema wamepiga hatua kubwa baada ya mabadiliko ya sheria iliyoruhusu kuanzishwa kwa Kampuni za kukusanya na kugawa mirabaha nchini. 

Amesema hadi sasa Kampuni ya Society of Music and Advocacy (SOMA) inasimamia ukusanyaji wa mirabaha kwa darala la kazi za Muziki na Kampuni ya Tanzania Reproduction Rights Society Limited (TANRRS) inasimamia ukusanyaji wa mirabaha kwa kazi za Maandishi. Alisema hata hivyo, bado wanakabiliwa na changamoto ya baadhi ya watumiaji kutotaka kuzingatia takwa la kisheria la kulipia leseni za matumizi ya kazi hizo.

Amesema kikao hicho kinalenga kuondoa mivutano hiyo na kuweka utaratibu wa pamoja wa kufuata sheria bila shuruti, ili kuhakikisha kuwa mirabaha hii ya muzikiinayochangia ukuaji wa biashara zao pamoja na kuleta burudani, inamneemesha pia alieitengeneza.

Aidha, amesema hadi kufikia sasa, kupitia miongozo ya Wizara wameweza, kuongeza idadi ya wasanii waliosajiliwa na kuhifadhi za kazi zao na Kuimarisha ushirikiano na wadau wa kimataifa kama kushirikiana na  Flora ROUSSEAU, Balozi wa BASATA, Ndugu Rob Hooijer, Mshauri wa masuala ya Hakimiliki na Hakishiriki Afrika, katika kukuza uelewa wa hakimiliki. 

 Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Habari Sanaa Utamadini na  Michezo, Gerson Msigwa Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo na Sanaa wa wizara  hiyo Dk. Emmanuel Ishengoma amesema hakuna shaka juu ya muziki unaotengenezwa nchini pamoja na maudhui yake.

Amesema serikali ipo tayari kuwasaidia Wadau kufikia malengo, ili wanamziki wapate kipato kutokana na jasho lao wanololitoa katika ubunifu.

"Hawa wabunifu halali wanalala wakibuni tufanye nini ili kuwe na tofauti na mziki uliotoka jana usimezwe lakini jambo baya tunaweza kutumia kazi zao bila kuwalipa kwa kisingizio kama tunawapromote sio kitu kizuri mtu awe maarufu halafu hana kitu.

"Mziki unaonchezwa kwenye baa, kumbi za mahoteli, magari sio kelele ni mali inayowafanya wateja wajiskie amani na kuvurudika 

"Utaona kwamba mauzo ya bia yanasindikizwa na kitu kingine Kuna mmoja aliwahi kuja kulalamika wanatutoza hela kupiga mziki katika baa nikamwambia ...acha kuweka mziki. Muziki ndio roho ya sehemu nyingi za starehe mfanyabiashara atambue kwamba starehe hiyo ina gharama" amesema Dk.Ishengoma