Ruto kutoa mbinu dhidi ya uhaba wa makazi

By Mwandishi Wetu , Nipashe Jumapili
Published at 03:31 PM May 17 2026
Rais wa Kenya, William Ruto
Picha: Mtandao
Rais wa Kenya, William Ruto

Rais wa Kenya, William Ruto, yupo mjini Baku, Azerbaijan kuhudhuria mkutano wa kimataifa wa upanuzi wa miji (World Urban Forum), akitarajiwa kuonesha mpango wake wa ujenzi wa makazi ya bei nafuu kama mojawapo ya njia za kukabiliana na uhaba wa makazi duniani.

Mpango huo wa ujenzi wa makazi ya bei nafuu, aliuanzisha pindi tu alipochaguliwa 2022, ingawa ulipingwa mahakamani na baadhi ya wakenya ambao walihisi kuwatoza wafanyakazi kodi ya asilimia 1.5 ya mshahara kufadhili mradi huo ilikuwa kinyume cha sheria.

Mahakama ilisimamisha mpango huo kwa muda kabla ya bunge kupitisha muswada wa serikali na kuifanya kuwa sheria kwa wafanyakazi kulipa kodi ya makazi almaarufu (Affordable Housing levy).

Kwa mujibu wa Wizara ya Ujenzi na Nyumba, Idara inayosimamia mpango wa ujenzi wa makazi ya bei nafuu imerekodi kwamba nyumba 111,975 zimekamilishwa katika kaunti 47 nchini Kenya, huku wanunuzi wakijiandikisha katika mpango wa Boma Yangu na kulipa pole pole kwa kipindi cha miaka 30.

Katika kikao cha makazi kinachoandaliwa nchini Azerbaijan kati ya May 17 na 22, Kenya inajiandaa kuonesha jinsi serikali za mataifa mengi duniani zinavyoweza kutumia ufadhili wa ndani kukabiliana na uhaba wa makazi. 

Afrika miongoni mwa maeneo yenye uhaba wa makazi na yakiwapo ni duni
Rais Ruto anasema kupitia mpango wa nyumba za bei nafuu, anakabiliana na makazi duni yaliyopo katika miji kadhaa ikiwemo Nairobi ambapo ina mitaa kadhaa ya mabanda.

Mkutano wa kwanza wa makazi wa kimataifa uliandaliwa Kenya mnamo 2002.

Chanzo: BBC