Majonzi kwa wazazi, walezi wakiitambua miili ya watoto wao

By Mwandishi Wetu , Nipashe Jumapili
Published at 01:14 PM May 31 2026
Wahudumu wa Msalaba Mwekundu wakitoa miili ya wanafunzi walioathirika kwenye mkasa wa moto
PICHA: Taifa Leo/BBC
Wahudumu wa Msalaba Mwekundu wakitoa miili ya wanafunzi walioathirika kwenye mkasa wa moto

Huzuni na majonzi zimetanda katika mochwari ya Hospitali ya Kaunti Ndogo ya Naivasha, huku familia, jamaa na marafiki wa wasichana 16 waliofariki katika mkasa wa moto katika Shule ya Upili ya Utumishi Girls wakianza shughuli ngumu ya kutambua miili ya wapendwa wao.

Tukio hilo lilifanyika jana, Moto huo uliteketeza bweni la Meline WaitheBlock B, usiku wa Jumatano.

Bweni hilo lilikuwa na wanafunzi 220 wa Gredi ya 10, Kidato cha Tatu na Kidato cha Nne. 

Wazazi wa wasichana hao 16, wakifuatana na jamaa zao, walifika hospitalini kwa shughuli ya uchunguzi wa maiti, huku wakifarijiana katika kipindi hiki kigumu ambacho kimeacha nchi katika maombolezo.

Madaktari watatu wa uchunguzi wa maiti wametumwa kuhakikisha zoezi hilo linakamilika haraka na kwa ufanisi. 

Uchunguzi huo unatarajiwa kusaidia kubaini chanzo halisi cha vifo hivyo pamoja na kurahisisha kutambua miili. 

Familia hizo pia zinasubiri matokeo ya vipimo vya DNA kabla ya kukabidhiwa miili kwa mazishi.

Nje ya hifadhi ya maiti, jamaa walionekana wakiwa wamelemewa na huzuni. 

Wanafamilia walifika eneo husika
Wengine walikuwa wakisali huku wengine wakikumbuka maisha ya wasichana hao ambao ndoto zao zilikatizwa ghafla na moto huo. 

Wasichana wengine saba waliopata majeraha bado wamelazwa katika hospitali moja jijini Nairobi.

Maofisa wa hospitali waliimarisha usalama katika eneo la mochwari, ili kudumisha utulivu wakati wa zoezi hilo muhimu. 

Ni wanafamilia wa karibu na wahudumu walioidhinishwa pekee kuingia.

Shirika la Msalaba Mwekundu Kenya pia limeweka mahema katika eneo hilo, washauri nasaha na wanasaikolojia wanatoa huduma kwa familia zilizoathirika. 

Magari mawili ya ambulensi yamewekwa tayari kushughulikia dharura zozote za kiafya.

Baada ya kuona miili hiyo, mmoja wa jamaa, Njuki Nthimba, amesema ni miili mitatu pekee iliyoweza kutambuliwa kwa urahisi huku mingine ikiwa imeungua vibaya kiasi cha kutotambulika.

Chanzo: Taifa Leo