Wachimbaji wadogo wa madini nchini wametakiwa kuachana na dhana za ushirikina, ikiwemo imani kuwa mwanamke akiwa kwenye siku zake anaweza kusababisha kupotea kwa madini, na badala yake kutumia teknolojia na zana za kisasa ili kuongeza tija katika uchimbaji.
Wito huo umetolewa na Afisa Programu wa Taasisi ya kuendeleza uchimbaji mdogo Tanzania (FADev), Rehema Mkuli, wakati wa mafunzo kwa wachimbaji wa madini ya ujenzi na viwandani yaliyofadhiliwa na United Nations Development Programme kupitia mradi unaotekelezwa katika mikoa ya Singida, Dodoma, Morogoro na Tanga.
Amesema mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo wachimbaji kusoma ramani za kijiolojia, kutumia mifumo ya GPS na kupata taarifa sahihi za miamba ili kuboresha uchimbaji na kuondokana na imani potofu.
Mtaalamu wa miamba na madini kutoka Ofisi ya Madini Mkoa wa Morogoro, Asifiwe Ngala, amesema matumizi ya ramani za kijiolojia husaidia kutambua muundo wa miamba, kuepuka uchimbaji holela na kulinda mazingira.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa kikundi cha wachimbaji madini ya dolomite (Tushikamane), Ramadhani Madenge, ameomba wadau kuwasaidia kupata vifaa vya kijiolojia ili kuboresha uzalishaji.
Naye mchimbaji mdogo, Mwanzani Juma, ameomba serikali kuongeza bei ya dolomite kutoka Sh1,500 hadi Sh3,000 kwa debe ili kuwawezesha kujikwamua kiuchumi.
Mafunzo hayo yameelezwa kuwa sehemu ya juhudi za kuboresha shughuli za wachimbaji wadogo na kuongeza mchango wao katika uchumi wa taifa.
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED