TANZANIA imeendelea kujipambanua kama kitovu kipya cha uwekezaji katika sekta ya dawa barani Afrika baada ya kuvutia wawekezaji wa kimataifa katika Maonesho ya Kimataifa ya Dawa ya CPHI China 2026 yaliyofanyika jijini Shanghai, China.
Kupitia ushiriki wake katika maonesho hayo makubwa yaliyofanyika kuanzia Juni 16 hadi 18 mwaka huu katika Kituo cha Maonesho cha Shanghai New International Expo Center, Tanzania imewasilisha fursa mbalimbali za uwekezaji katika uzalishaji dawa, chanjo, malighafi za dawa na vifaa tiba kwa lengo la kuifanya nchi kuwa kitovu cha uzalishaji bidhaa za afya kwa soko la Afrika.
Ujumbe wa Tanzania uliongozwa na Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Dawa na Vifaa Tiba, Emmanuel Tayari, ukiwakilisha Kikosi Kazi cha Kuharakisha Uwekezaji katika Sekta ya Dawa na Vifaa Tiba (Pharmaceutical Investment Acceleration Taskforce – PIAT).
Katika siku za mwanzo za maonesho hayo, banda la Tanzania lilikuwa kivutio kikubwa kwa wawekezaji kutoka mataifa mbalimbali waliotaka kufahamu kwa undani mazingira ya uwekezaji yaliyopo nchini.
Wawekezaji hao wameonesha nia ya kuwekeza katika viwanda vya dawa za kawaida, dawa za sindano, chanjo, bidhaa za kibaolojia pamoja na uzalishaji malighafi za dawa zinazotumika katika kutengeneza bidhaa mbalimbali za afya.
Mwitikio huo unaashiria kuongezeka kwa imani ya wawekezaji wa kimataifa katika mageuzi yanayoendelea kufanywa na Serikali ya Tanzania katika kuimarisha sekta ya dawa na vifaa tiba.
Kupitia maonesho hayo, Tanzania imeeleza hatua mbalimbali zilizochukuliwa kuboresha mazingira ya uwekezaji, ikiwamo kuimarisha mifumo ya udhibiti wa dawa, kuweka vivutio vya uwekezaji, kuboresha mifumo ya ununuzi wa bidhaa za afya zinazozalishwa ndani ya nchi pamoja na kuanzisha maeneo maalumu ya viwanda vya dawa.
Tayari Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa, ameshasema kuwa Tanzania imejipanga kikamilifu kuwa moja ya vituo vikuu vya uzalishaji dawa barani Afrika.
“Tanzania iko tayari kuwa kitovu cha uzalishaji dawa barani Afrika. Mwelekeo uko wazi. Dhamira ni thabiti. Wakati ni sasa,” Waziri Mchengerwa anasema.
Tanzania inaingia katika majadiliano hayo ikiwa na soko linalokua kwa kasi kubwa. Takwimu zinaonesha mahitaji ya dawa nchini yanatarajiwa kuongezeka mara 4.6 ndani ya kipindi cha miaka 15 ijayo.
Mahitaji hayo yanakadiriwa kuongezeka kutoka pakiti milioni 131 katika mwaka wa fedha 2024/25 hadi zaidi ya pakiti milioni 600 ifikapo mwaka wa fedha 2039/40.
Ongezeko hilo linachochewa kwa kiasi kikubwa na utekelezaji mpango wa Bima ya Afya kwa Wote unaolenga kuongeza upatikanaji huduma za afya kutoka takribani asilimia nane ya Watanzania wa sasa hadi asilimia 62 ndani ya miaka mitano ijayo.
Katika mazungumzo yake na wawekezaji, Tanzania imeendelea kusisitiza uimara wa mfumo wake wa udhibiti wa dawa kupitia Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba Tanzania (TMDA), ambayo imekuwa mamlaka ya kwanza ya kitaifa barani Afrika kufikia Kiwango cha Tatu cha Ukomavu (WHO Maturity Level 3) kilichowekwa na Shirika la Afya Duniani (WHO).
Vilevile, muda wa usajili wa bidhaa zinazozalishwa nchini umepunguzwa hadi siku 60, hatua inayolenga kupunguza urasimu na kuharakisha uwekezaji.
Serikali pia imeeleza kuwa kupitia Bohari ya Dawa (MSD), bidhaa za afya zenye thamani ya takribani dola za Marekani milioni 491 hununuliwa kila mwaka kwa ajili ya kuhudumia zaidi ya vituo 8,800 vya kutolea huduma za afya nchini.
Mbali na hilo, wazalishaji wa ndani wanapatiwa upendeleo wa bei wa asilimia 15 katika zabuni za serikali pamoja na mikataba ya muda mrefu ya usambazaji bidhaa za afya.
Katika kuimarisha zaidi mazingira ya uwekezaji, serikali imeainisha maeneo maalumu ya viwanda vya dawa katika Mloganzila na Kibaha, huku ikiwekeza dola za Marekani milioni 10 kwa ajili ya maabara ya kisasa ya pamoja ya upimaji ubora wa dawa na tafiti za ulinganifu wa kibaolojia (bioequivalence laboratory).
Kupitia mfumo wa Green-Lane Fast Track, wawekezaji wanaowekeza katika sekta ya dawa sasa wanapata huduma za leseni, ardhi, kodi, usajili wa bidhaa na masuala ya udhibiti kupitia mfumo mmoja unaorahisisha taratibu na kupunguza muda wa kusubiri maamuzi.
Ujumbe wa Tanzania pia unalenga kuvutia uwekezaji katika uzalishaji wa malighafi za dawa (Active Pharmaceutical Ingredients – APIs) na viambata vingine muhimu vya dawa, eneo ambalo bado halina uzalishaji wa ndani katika nchi zote za Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Maeneo mengine yaliyowekwa katika vipaumbele vya uwekezaji ni pamoja na uzalishaji wa chanjo, bidhaa za kibaolojia, dawa za sindano za ujazo mdogo na dawa muhimu zinazozalishwa kwa viwango vya WHO-GMP.
Wadau wa sekta ya afya wanaona kuwa uwekezaji katika maeneo hayo unaweza kuifanya Tanzania kupunguza utegemezi wa uagizaji wa dawa kutoka nje ya nchi huku ikiimarisha usalama wa upatikanaji wa bidhaa za afya kwa wananchi.
Tanzania pia imeendelea kujinadi kama lango la biashara ya dawa kwa ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini kutokana na uanachama wake katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).
Kupitia masoko hayo mawili, bidhaa za dawa zinazozalishwa nchini zinaweza kufikia soko la watu zaidi ya milioni 780, fursa inayotajwa kuwa moja ya vivutio vikubwa kwa wawekezaji wa kimataifa.
Fursa hizo zinatarajiwa kuongezeka zaidi kupitia utekelezaji Mkataba wa Wakala wa Dawa Afrika (African Medicines Agency), ambao unalenga kurahisisha biashara ya dawa na kuimarisha ushirikiano wa udhibiti wa dawa barani Afrika.
Katika kuthibitisha dhamira ya serikali kulinda wawekezaji wa ndani na nje wanaozalisha bidhaa kwa viwango vinavyokubalika, Waziri Mchengerwa amekuwa akisisitiza kuwa Tanzania haitaruhusu ushindani usio wa haki kutoka kwa bidhaa zinazoagizwa kutoka nje.
“Hakuna mwekezaji atakayeombwa kujenga viwanda Tanzania halafu akakwama kutokana na ushindani usio wa haki wa bidhaa zinazoagizwa kutoka nje. Enzi hizo zimekwisha,” amesema Waziri Mchengerwa.
Kauli hiyo imeendelea kuwapa matumaini wawekezaji wanaotafuta maeneo salama ya kuwekeza katika uzalishaji dawa, huku Tanzania ikiibuka kama moja ya nchi zinazochukua hatua za makusudi kujenga sekta imara ya dawa na vifaa tiba inayoweza kuhudumia mahitaji ya ndani na ya kikanda.
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED