Wakati athari za mabadiliko ya tabianchi zikizidi kutikisa maisha ya wananchi wanaotegemea bahari, Zanzibar inakuwa mwenyeji wa mkutano mkubwa wa kimataifa unaowakutanisha watafiti, watunga sera, wanataaluma na viongozi wa sekta binafsi kujadili hatma ya uchumi wa buluu na namna ya kugeuza changamoto kuwa fursa za maendeleo.
Warsha hiyo ya 29 ya mwaka kuhusu mageuzi ya uchumi wa buluu,itawakutanisha washiriki kutoka ndani na nje ya Tanzania, huku nchi mbalimbali ikiwemo Uholanzi, Norway, Sweden, Denmark, Seychelles, Mauritius, Namibia, Afrika Kusini na Indonesia zikitarajiwa kushiriki katika mjadala huo wa siku mbili unaofanyika kesho visiwani humo.
Akizungumza na waandishi wa habari, Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi, Kapteni Hamad Bakari, amesema Zanzibar inaendelea kukumbwa na athari kubwa za mabadiliko ya tabianchi zinazohatarisha sekta muhimu za uchumi wa wananchi, hususan uvuvi, kilimo na uzalishaji wa mwani.
Amesema ongezeko la joto la maji ya bahari limeanza kuathiri uzalishaji wa mwani baada ya zao hilo kushindwa kuota katika kina kifupi cha maji kama ilivyokuwa hapo awali. “Hivi sasa wakulima wengi wanalazimika kwenda katika kina kikubwa zaidi kutokana na joto la maji kuongezeka,” amesema.
Kapteni Hamad amesema hali hiyo pia imeathiri matumbawe ambayo ni mazalia muhimu ya samaki, jambo linalopelekea samaki kuhama kutoka maeneo ya karibu na ufukwe kwenda maji ya kina kirefu na kuwaacha wavuvi wadogo wakikosa mavuno ya kutosha.
Aidha amesema kuongezeka kwa kina cha maji ya bahari kutokana na kuyeyuka kwa barafu duniani kumeanza kuingiza maji ya chumvi katika mashamba ya mpunga na kusababisha baadhi ya wakulima kushindwa kuendelea na kilimo hicho.
Ameleza licha ya changamoto hizo, Zanzibar bado ina nafasi kubwa ya kunufaika na uchumi wa buluu kwa kutumia maeneo yaliyoathirika kwa shughuli mbadala za kiuchumi kama ufugaji wa samaki, kamba, kasa na majongoo bahari.
“Baadhi ya nchi zilizokumbwa na athari kama hizi zimefanikiwa kubadili changamoto kuwa fursa kupitia ufugaji wa mazao ya baharini,” alisema.
Mkurugenzi wa Utafiti kutoka Taasisi ya Utafiti ya REPOA, Jamal Msami, amesema warsha hiyo inalenga kuibua mapendekezo mahsusi ya sera yatakayosaidia kuimarisha uchumi wa buluu na kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 pamoja na Dira ya Maendeleo ya Zanzibar 2050.
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED